In Summary
  • Haijabainika kwa nini wazazi hawakumtaka mkuu huyo mpya wa shule
  • Ogaga alikuwa aanze rasmi kutekeleza majukumu yake baada ya kutambulishwa shuleni Alhamisi

Wanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Otok Mixed eneo bunge la Karachuonyo mnamo Alhamisi waliwapiga viboko na kuwafukuza baadhi ya wazazi kwa madai ya kushambulia mwalimu mkuu wa shule yao.

Wanafunzi hao walipiga kundi la wazazi waliovamia  shule hiyo na kumtimua mwalimu wao mkuu Jactone Ogaga.

Walitumia fimbo za mbao na mawe kuwavamia wazazi hao ambao waliwatuhumu kusababisha fujo na kuingilia masomo yao.

Inaarifiwa kuwa wazazi hao hawakutaka Ogaga kufundisha na kutekeleza usimamizi wa shule hiyo.

Haijabainika kwa nini wazazi hawakumtaka mkuu huyo mpya wa shule.

Ogaga alikuwa aanze rasmi kutekeleza majukumu yake baada ya kutambulishwa shuleni Alhamisi.

Kizaazaa kilianza pale baadhi ya wazazi walipoingia langoni na kuanza kuzomea huku wakimrushia matusi Ogaga.

Akizungumza baada ya tukio hilo, Ogaga alisema wanafunzi walitoka katika madarasa yao wakati baadhi ya wazazi walianza kurushiana matusi.

Wakati wa vurugu hizo, naibu mkuu wa shule alijeruhiwa baada ya kupigwa na jiwe.

Baadhi ya wanafunzi wenye hasira walichukua vijiti vya mbao na kuzipiga. Wazazi walifukuzwa hadi takriban kilomita 2 kutoka shuleni,” Ogaga alisema.

Naibu mkuu wa shule bado anaendelea na matibabu katika kituo cha afya kilicho karibu. Wanafunzi waliozungumza na wanahabari walilalamika kuwa baadhi ya wazazi hawataki shule hiyo iendelee.

"Siku zote wanataka walimu wazuri wahamishwe lakini kwetu sisi, tunataka kufundishwa na kufaulu katika taaluma," mwanafunzi alisema.

Waliwashutumu wazazi hao kwa kuingia kwa nguvu shuleni.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Rachuonyo Kaskazini Lydia Parteiyie alisema wamewakamata wazazi watatu.

"Tunawahoji washukiwa ili kubaini sababu kwa nini walitaka kumfukuza mkuu wa shule," Parteiye alisema.

 

 

 

 

View Comments