In Summary

• Naibu chansela alisema hatua hiyo ni kutoa nafasi kwa wanafunzi na wafanyikazi kujituliza akili na kukubali kilichotokea.

Chuo cha Pwani chafungwa kufuatilia ajali ya basi la chuo hicho.
Image: Twitter

Uongozi wa chuo kikuu cha Pwani umetoa barua ya ghafla kwa wafanyikazi na wanafunzi wa chuo hicho kuondoka kuelekea nyumbani mara moja.

Kufungwa huko kumechochewa na ajali mbaya ya basi la chuo hicho kule Naivasha ambayo iligharimu watu 18, wakiwemo wanafunzi waliokuwa wanaelekea katika hafla ya michezo Eldoret na baadhi ya wafanyikazi wa chuo.

Katika barua hiyo ambayo imeonekana na Radio Jambo, naibu chansela alisema kwamba amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya mashauriano ya kina na washikadau na wakaafikia kuwa huenda wanafunzi hawatakuwa katika hali sawa ya kiakili kufanya mitihani ijayo, na hivyo kuona kuna haja ya kuwapa mapumziko ya lazima kwa wiki mbili ili kupisha maombolezo.

“Kufuatia ajali mbaya iliyohusisha basi la chuo mnamo Machi 30 kule Naivasha likiwasafirisha wanafunzi kwenda michezo ya vyuo Eldoret, imetambulika kwamba shughuli za masomo zimeathirika pakubwa chuoni. Zaidi ya hayo, wanafunzi huenda hawatakuwa sawa kifikira na kimawazo kufanya mitihani ijayo ya mwisho wa muhula.”

“Kutokana na hilo, chuo kiliketi mkutano Aprili mosi na kuamua kujipanga upya kwa muhula huu ili kupisha kipindi cha maombolezo na kutafuta ushauri nasaha ili kufikia hatua ya kukubali kilichotokea. Hivyo wanafunzi wanatakiwa kufanay mipango ya kusafiri nyumbani kuanzia Aprili 1 na chuo kitasalia kufungwa hadi Aprili 17,” sehemu ya barua hiyo ilisoma.

Basi la chuo hicho liligongana na gari dogo la kubeba abiria eneo la Kayole katika barabara ya Naivasha kuelekea Nakuru mapema Jumatatu na kughariu maisha ya watu wasiopungua idadi ya 17.

View Comments