In Summary

• Dan Mackenzie anasema kuwa baba yake alimuarifu kuwa anaelekea Shakahola kuanza ukulima baada ya kanisa lake kufungwa.

•Dan aliongeza pia alikua akishiriki katika kanisa hilo la Good News International na hata kuhudumu kama mpiga picha wakati wa kupeperusha mahubiri ya kanisa hilo kupitia televisheni.

MCHUNGAJI PAUL MACKENZIE
Image: ALPHONSE NGARI

Mwanawe mhubiri Paul Mackenzie anayeshtakiwa kwa madai ya vifo ya watu 110 katika Kijiji cha Shakahola ajitokeza na kumtetea baba yake huku akisema kuwa baba yake aliacha kuhubiri baada ya kanisa lake la Good life international kufungwa mwaka wa 2019.

Dan Mackenzie mwenye umri wa miaka 21 anayefanya kazi kama mwana bodaboda katika mji wa Malindi anasema kuwa baba yake alimuarifu kuwa anaelekea Shakahola kuanza ukulima baada ya kanisa lake kufungwa.

“Alisema kuwa anaenda kununua shamba mbele ya Shakahola pale, anaenda kulima. Kwa hivyo nikamwambia ni sawa mimi si mkulima acha nibaki mjini nifanye kazi zangu” alisema Dan

Dan aliongeza pia alikua akishiriki katika kanisa hilo la Good News International na hata kuhudumu kama mpiga picha wakati wa kupeperusha mahubiri ya kanisa hilo kupitia televisheni.

“Hayo yote ni uongo kwa sababu yeye hakuenda kule Shakahola na washirika alienda peke yake na alienda kununua shamba kule peke yake, kwa sababu alikua anataka kulima kwa kuwa alikua mkulima tangia mwaka wa 2015” Dan aliongeza.

Paul Mackenzie, ambaye ni kiongozi wa Kanisa la Good News International, anakabiliwa na makosa makubwa ya mauaji, kushauri na kusaidia watu kujiua, utekaji nyara, kuendeleza itikadi kali, mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, ukatili wa watoto, utapeli, ulaghai miongoni mwa mengine.

Ijumaa, timu ya mashtaka inayoshughulikia kesi dhidi yake iliomba mahakama kuruhusu serikali kumzuilia mshukiwa, na washtakiwa wenzake, kwa siku 90 zaidi ili kuruhusu kukamilika kwa uchunguzi.

View Comments