In Summary
  • Pia alitupilia mbali ripoti zinazodai kuwa alihongwa ili kumuunga mkono Ruto na mapendekezo yake ya hatua za ushuru zilizoainishwa katika Mswada wa Fedha wa 2023.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Image: Facebook

Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi, Esther Passaris, mnamo Alhamisi, Juni 15, alipuuza ripoti zinazodai kwamba ameshawishiwa kuacha muungano wa Azimio la Umoja ili kujiunga na serikali chini ya Rais William Ruto.

Passaris, ambaye alizungumza nje ya Bunge baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya 2023/24, alishikilia kuwa bado alikuwa mwanasiasa mahiri wa Orange Democratic Movement (ODM) na mfuasi mkubwa wa Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Pia alitupilia mbali ripoti zinazodai kuwa alihongwa ili kumuunga mkono Ruto na mapendekezo yake ya hatua za ushuru zilizoainishwa katika Mswada wa Fedha wa 2023.

"Bado niko Azimio na nimekuwa ODM tangu 2007. Nimemuunga mkono Raila tangu wakati huo, ambaye ametuunga mkono kama wagombea," Passaris alitetea msimamo wake.

Kuhusu kupigia kura Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 na kukataa kuungana na wenzake kutoka Bungeni wakati bajeti ikiwasilishwa, Passaris alieleza kuwa serikali inahitaji fedha kwa ajili ya shughuli zake.

Wakati uo huo, alipongeza utawala wa Kenya Kwanza kwa kuongeza mgao wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB) na kutenga Ksh141 bilioni kwa sekta ya Afya. HELB itapokea Ksh30 bilioni, kutoka Ksh15 bilioni, katika bajeti ya kwanza ya Ruto.

"Ningependa kusema kwamba serikali yoyote haiwezi kufanya kazi bila fedha. Nchi yetu inakabiliana na madeni makubwa, na hatutaki wakopeshaji kuchukua hatua za kubana matumizi kudhibiti hilo.

“Kwa hiyo tusimame kidete kuhakikisha Serikali yetu inakuwa na fedha, fedha hizo ikiwa Serikali haitakusanya kodi tutazipata wapi, watu lazima walipishwe kodi ili Serikali nayo itimize wajibu wake, nimeona mambo mazuri kutoka kwa bajeti, ikijumuisha ongezeko la mgao kwa HELB na hospitali," Passaris alisema.

"Bado niko upinzani na nitahakikisha kuwa pesa zote zimehesabiwa ipasavyo," alisisitiza.

ODM ilitangaza kuwa itawachukulia hatua za kinidhamu wanachama wake waliounga mkono Mswada wa Fedha wa 2023 na mchakato wa kusoma bajeti. Passaris na Mbunge wa Lang'ata, Phelix Odiwour (Jalang'o), waliorodheshwa miongoni mwa wabunge waliolengwa.

 

 

 

 

 

View Comments