In Summary

• Wiki iliyopita, Brownskin alizuiliwa baada ya upande wa mashtaka kusema ripoti yake ya awali ya dhamana haikuwa tayari.

• Mcheza santuri huyo amekanusha shtaka la kusaidia kujiua kwa mkewe Sharon Njeri Mwangi mnamo Julai 29, 2022.

Dj Brownskin katika Mahakama ya Milimani mnamo Juni 14, 2023.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Michael Macharia Njiiri almaarufu DJ Brownskin anayedaiwa kuhusika katika kisa cha kujitoa uhai kwa mkewe mwaka jana ameachiliwa kwa bondi ya shilingi 200,000.

Jumatatu, hakimu mkuu wa Milimani, Lukas Onyina alisema alizingatia ripoti ya awali ya dhamana ambayo alisema ilimpendelea.

"Nimezingatia ripoti iliyo mbele yangu ambayo inampendelea mshtakiwa kwani yeye si hatari ya kukimbia endapo ataachiliwa. Ninampa bondi ya shilingi 200,000 au dhamana ya pesa taslimu shilingi 100,000," hakimu alisema.

Onyina aliamuru kuwa kesi hiyo itatajwa tena  mnamo Juni 22, 2023.

Wiki iliyopita, Brownskin alizuiliwa baada ya upande wa mashtaka kusema ripoti yake ya awali ya dhamana haikuwa tayari.

Mahakama hiyo ilikataa kuruhusu ombi la DJ Brownskin ambalo alitaka afisa wa DCI katika eneo la Kasarani aitwe kortini kwa kutotii amri la koti.

Kupitia kwa wakili wake Duncan Okatch, DJ huyo alikuwa ameomba afisa wa DCI Jimmy Kimaru aitwe kufika kortini kwa kukiuka maagizo ya mahakama  ya Makadara wiki jana ambayo yalimwachilia huru.

Hata hivyo, katika uamuzi wa Onyina, mahakama hiyo ilisema kuwa haiwezi kuthibitisha kosa lolote la ukiukaji wa amri za mahakama zinazodaiwa kukiukwa zilizotolewa na Mahakama ya Sheria ya Makadara ambayo ina mamlaka sawa.

Hakimu alibainisha kuwa Njiiri alifikishwa mbele ya mahakama yake kujibu madai ya kusaidia kujitoa uhai.

Baada ya ombi hilo, wakili wake aliiomba mahakama hii kutoa wito dhidi ya afisa huyo wa DCI Kasarani, akitaja ukiukaji wa maagizo ya mahakama.

Alisema wakili wa mshtakiwa alidai kuwa mteja wake alilazimishwa kukiri kosa hilo ikiwa ni sharti la kuachiliwa kwake.

Wakili wa upande wa mashtaka aliiambia mahakama hii kuwa masuala yaliyotolewa na upande wa utetezi yanatokana na faili tofauti zilizopo katika Mahakama ya Sheria ya Makadara hivyo ni mahakama ya Makadara pekee yenye uwezo wa kushughulikia ombi hilo.

"Nakubaliana na upande wa mashtaka kwamba kwa hakika jalada lililo mbele ya mahakama hii halina dharau yoyote. Hivyo basi, naelekeza wakili wa utetezi kupelekea Mahakama ya Makadara kwa maombi ya kumwita DCIO endapo itaona inafaa," iliamuru Mahakama hiyo.

Mcheza santuri huyo amekanusha shtaka la kusaidia kujiua kwa mkewe Sharon Njeri Mwangi mnamo Julai 29, 2022.

Alikabiliwa na shtaka la pili la kukosa kutumia nguvu zote kumzuia mkewe asijiue ingawa alijua kwamba alikuwa akipanga kujiua.

Alishtakiwa zaidi kwa kuharibu ushahidi wa kujitoa uhai kutoka kwa simu yake mnamo Juni 1, 2023, akijua kuwa ushahidi huo utahitajika katika kesi za mahakama.

View Comments