In Summary
  • Nao wabunge 72 walipiga kura ya LA kupinga pendekezo hilo linaloungwa mkono na Rais William Ruto.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Image: Facebook

Baada ya mjadala mkali, wabunge mnamo Jumatano usiku walipitisha ushuru wa nyumba wa kima cha asilimia 1.5 ya mishahara ya wafanyakazi kila mwezi.

Katika kura ya moja kwa moja iliyopigwa kwa pendekezo hilo lililowasilishwa na Kamati ya Bunge kuhusu Fedha, wabunge 184 walipiga kura ya NDIO, wengi wao wakiwa wabunge wa Kenya Kwanza.

Nao wabunge 72 walipiga kura ya LA kupinga pendekezo hilo linaloungwa mkono na Rais William Ruto.

“Matokeo ya upigaji kura kuhusu pendekezo hilo la marekebisho kwa Mswada wa Fedha wa 2023 yanaonyesha upande wa NDIO umepata kura 184 huku wabunge 72 wakipiga kura ya LA kupinga pendekezo hilo,” akasema Spika wa muda David Ochieng.

Kupitishwa kwa ushuru huu sasa kunaashiria kuwa wafanyakazi wote watakuwa wakilipa ushuru wa kima cha asilimia 1.5 kwa mishahara yao kuanzia Julai 1, 2023.

Nao waajiri wao watalipa kiasi kama hicho cha mishahara ya wafanyakazi wao kila mwezi.

Pesa hizi zitawekwa katika Hazina ya Nyumba kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Ushuru huu, bila shaka utaongeza gharama kwa waajiri hali itakayosababisha baadhi yao kupunguza idadi ya wafanyakazi.

Nao wafanyakazi, ambao tayari wanazongwa na mzigo wa gharama ya maisha, pia watafinyika zaidi na ushuru huu mpya.

Hata hivyo, Rais Ruto amesisitiza kuwa mpango huu utasaidia kuzalisha takriban nafasi milioni mbili za ajira kila mwaka, hali ambayo itachochea ukuaji wa kiuchumi.

Mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Nairobi licha ya kuwa kwenye muungano wa Azimio ambao unapinga mswada huo, aliunga mkono ushuru wa nyumba.

Huku akizungumzia na kutoa sababu ya kuunga mkono alisema;

"Nina ndoto ya Kenya ambapo taswira ya vitongoji duni imesalia katika vitabu vyetu vya historia na sio katika nchi yetu mama. Kwa mamilioni ya Wakenya wanaoishi katika vitongoji duni 1,400+, nilipiga kura ya NDIYO kuhusu Ushuru wa nyumba.

Kwa sababu pamoja tunaweza kuwa walinzi wa kaka na dada zetu. Kumbuka ni msaada wako wa nyumbani; dereva; mjumbe; mlinzi; jamaa wa mbali; nk wanaoishi katika makazi duni. 1.5% sio ombi kubwa la kubadilisha maisha kupitia kuishi kwa heshima. #KushirikiNiKujali #Rasilimali za Kuvuta,"Amesema mbunge huyo.
View Comments