In Summary

• Mswada huo ulikuwa na mapendekezo 87 ya marekebisho, baadhi yakiwa yameidhinishwa Jumanne iliyopita, huku Bunge likizijadili hadi usiku wa manane.

• Katika mapendekezo ya bajeti hiyo, shilingi trilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 718 kwa ajili ya maendeleo huku shilingi bilioni 986  zikitumika kulipia deni la umma.

Rais William Ruto aidhinisha Mswada wa Fedha wa 2023 Ikulu Juni 26, 2023.
Image: PCS

Rais William Ruto Jumatatu ametia saini mswada wa fedha wa 2023 na kuifanya iwe sheria baada ya wabunge kuidhinisha hatua za ushuru zinazolenga kufikisha lengo la shilingi trilioni 3. 6.

Wabunge siku ya Jumatano,Juni 21 ,usiku walipitisha Mswada wa Fedha uliopendekezwa na Rais Ruto licha ya malalamishi ya Wakenya wengi.

Hii itakuwa bajeti ya kwanza kwa utawala wa Kenya Kwanza ambao umetanguliza nguzo tano chini ya ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi ya Bottom-Up.

Bajeti hiyo ya shilingi trilioni 3.6 itakuwa ikilenga kudumisha usawa kati ya kulipa deni na kuleta ukuaji wa uchumi.

Katika mapendekezo ya bajeti hiyo, shilingi trilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 718 kwa ajili ya maendeleo huku shilingi bilioni 986  zikitumika kulipia deni la umma.

Mswada huo ulipitishwa baada ya kusomwa kwa tatu na mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya fedha na mipango ya kitaifa Kuria Kimani.

Mswada huo ulipitishwa hata wakati upande wa upinzani na chama tawala cha kikishiriki katika mjadala mkali kuhusu mapendekezo yaliyomo katika mswada huo.

Mswada huo ulikuwa na mapendekezo 87 ya marekebisho, baadhi yakiwa yameidhinishwa Jumanne iliyopita, huku Bunge likizijadili hadi usiku wa manane.

Muhimu kati ya mapendekezo yaliyopitishwa ni ushuru wa asilimia 16 wa ongezeko la thamani kwenye mafuta, kutoka asilimia 8.

Angalau wabunge 184 - wengi wao kutoka Kenya Kwanza - waliunga mkono mswada huo isipokuwa Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, huku wabunge 88 - wengi wao kutoka Azimio - walipinga vikali marekebisho hayo.

Tozo ya Makazi yenye utata, ambayo awali ilipendekezwa kuwa asilimia 3 pia ilipitishwa baada ya kufanyiwa marekebisho hadi asilimia 1.5 ya malipo ya jumla. Pendekezo hilo sasa limegeuzwa kuwa kodi.

Pendekezo la awali lilitaka ushuru huo uwe wa kuchanga na baada ya kipindi cha miaka 7 Wakenya wangeweza kupata hela walizokuwa wakichanga katika mpango huo.

Ushuru wa watayarishi wa maudhui ya kidijitali utatozwa kwa asilimia 5. Hapo awali, hii ilipendekezwa kuwa asilimia 15 na ukaweza kuibua upinzani mkali kutoka kwa waunda maudhui kote nchini wakiongozwa na mchekeshaji Erick Omondi.

View Comments