In Summary

• KFS imetetea uamuzi wa Ruto wa kuondoa marufuku ya takriban miaka sita ya kukata miti licha ya wasiwasi ulioibuliwa na wanaharakati wa mazingira.

• Jumapili, Ruto alisema hatua hiyo "ilicheleweshwa kwa muda mrefu" na inalenga kubuni nafasi za kazi na kufungua sekta za uchumi zinazotegemea mazao ya misitu.

Image: KENYA FOREST SERVICES

Shirika la Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS) limetetea uamuzi wa Ruto wa kuondoa marufuku ya takriban miaka sita ya kukata miti licha ya wasiwasi ulioibuliwa na wanaharakati wa mazingira.

Katika taarifa kwenye Twitter, Shirika hilo lilieleza bayana kuwa kuondolewa kwa marufuku ya ukataji miti katika misitu nchini kulitokana na uchunguzi ulioidhinishwa na waziri wa awali wa masuala ya mazingira na misitu.

Kulingana na KFS, uchunguzi huo ulifichua idadi kubwa ya mashamba ya misitu iliyokomaa na kupitisha ata ukomavu huo hivyo kuilazimu serikali kuingililia kati na kuweza kukata miti iliyo pitisha ukomavu wake na kuoza misituni.

“Spishi za miti ya kigeni zina muda wa mzunguko wa miaka 25 hadi 30 baada ya hapo ikiwa hazijavunwa, huanza kuoza. Hivyo KFS hutumia mipango ya ukataji miti kuvuna hadi hekta 5,000 kwa mwaka na hii inahakikisha Serikali inapata faida kutokana na uwekezaji katika Mashamba ya Misitu.

Jumapili, Ruto alisema hatua hiyo "ilicheleweshwa kwa muda mrefu" na inalenga kubuni nafasi za kazi na kufungua sekta za uchumi zinazotegemea mazao ya misitu.

“Hatuwezi kuwa na miti iliyokomaa inayooza kwenye misitu huku wenyeji wakiteseka kutokana na ukosefu wa mbao. Huo ni upumbavu,” alisema katika ibada ya kanisa huko Molo, mji ulio umbali wa kilomita 200 (maili 120) kaskazini magharibi mwa mji mkuu Nairobi.

"Ndio maana tumeamua kufungua msitu na kuvuna mbao ili tuweze kutengeneza ajira kwa vijana wetu na kufungua biashara."

Hatua hii ya Serikali ya Kenya Kwanza imewaacha Wakenya wakitoa hisia kinzani kuhusu swala hii, huku wengi wakilalamika kuwa hii ni unafiki kutoka kwa Rais kwani akiwa nje ya nchi anatetea hatua za kutunza mazingira na upande mwingine anondoa marufuku ya kukata miti.

View Comments