In Summary

• Wafuasi hao wamekuwa wakitupiwa vitoza machozi kutoka kwa polisi ambao wanaonekana kuhakikisha wanafunga barabara zote zinazoelekea katikati mwa jiji la Naiobi.

Polisi wawatupia vitoza machozi kwa wafuasi wa Azimio katika barabara ya Jogoo Julai 7,2023.
Image: EZEKIEL AMING'A

Msafara wa wafuasi wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga kuelekea Central Park wakakabiliwa na safari iliyojawa na machozi polisi wakijaribu kuwazuia kufika katikati ya mji.

Wafuasi hao wamekuwa wakitupiwa vitoza machozi kutoka kwa polisi ambao wanaonekana kuhakikisha wanafunga barabara zote zinazoelekea katikati mwa jiji la Naiobi.

Picha za moja kwa moja hadi saa 2:10 jioni zinaonyesha waandamanaji wakijaribu kufunika nyuso zao ili kupunguza athari za vitoza machozi kutoka kwa polisi.

Waandamanaji hao wanatembea kutoka eneo la Kamukunji kuelekea Gikomba ambapo wanatarajia kufikia barabara zinazoelekea CBD.

Wengine wanaonekana wakifunika mapua na sweta zao ili kuzuia gesi hiyo kuwaathiri. Licha ya shambulizi hilo wafuasi hao walonekana kutobabaishwa baada ya kupata maji ili kupunguza athari za gesi hiyo kali na kuendelea na safari yao.

Wakati fulani, mtu anasikika akiwataka maafisa wa polisi kufuata sheria.

"Mfuate sheria na msitumiwe vibaya tafadhali," anasema.

Katika viwanja vya Kamukunji, Raila aliwaamuru wafuasi wake kutumia njia yoyote inayowezekana kufika Central Park.

"Kuna njia nyingi za kufikia 'Rome', wakati wanazuia barabara moja, tunatumia nyingine. Leo, 'Rome' yetu inaitwa Central Park, hapo ndipo tutakutana baada ya mkutano wa Kamukunji," alisema.

Kiongozi huyo wa upinzani pia amewataka waandamanaji kukumbatia amani katika safari yao.

Takriban saa 2:36 jioni, msafara ulikuwa katika eneo la Ngara.

View Comments