In Summary
  • Waandalizi wa maandamano hayo wamesisitiza kuwa ni polisi waliochochea hali hiyo kuwa ya vurugu.
Wilson Sossion
Image: KWA HISANI

Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu nchini Kenya Wilson Sossion ametoa wito wa kuharamishwa kwa maandamano yote yaliyopangwa Jumatano.

Akizungumza Jumanne wakati wa mahojiano kwenye K24, Sossion alisema maandamano hayo hayaongezi thamani yoyote nchini.

"Kuanzia kesho (Jumatano), maandamano haya yote yawe ya uhalifu kwa sababu hayaongezi thamani yoyote kwa nchi. Hayo si maandamano, ni uhalifu," alisema.

Sossion alisema wakati wa maandamano hayo, Wakenya wengi hupoteza maisha na mali kuharibiwa hali inayosababisha hasara.

Alisema serikali inapaswa basi kuhakikisha maisha na mali zinatunzwa.

"Kupoteza maisha ni nyingi sana na mtu anapaswa kuwajibika. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa maisha yanalindwa, mali zinatunzwa na nchi salama," Sossion alisema.

Alisema upinzani una haki ya kuandamana lakini si kwa gharama ya Wakenya wengine.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki Jumatatu alithibitisha kwamba watu sita walipoteza maisha yao kufuatia maandamano ya Saba Saba yaliyoitishwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga.

"Ijumaa iliyopita, wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na muungano wa Azimio, watu sita waliuawa na wengine kujeruhiwa, wakiwemo maafisa wa usalama. Uhuru wa kujumuika na haki ya kuandamana/kunyang’anya mali haijumuishi haki ya kusababisha ghasia na kupora mali.” Waziri Kindiki alisema.

"Siku ya Jumatano, mtu yeyote anayetishia kufanya nchi isitawalike kupitia ghasia, uporaji, machafuko na umwagaji damu atashughulikiwa vilivyo, kwa mujibu wa sheria," alisema.

Waandalizi wa maandamano hayo wamesisitiza kuwa ni polisi waliochochea hali hiyo kuwa ya vurugu.

Maandamano hayo yaliitishwa kuadimisha siku ya Saba Saba, ambayo inahusishwa na mapambano ya nchi hiyo ya mfumo wa vyama vingi.

 

 

 

 

View Comments