In Summary
  • Katika ujumbe siku ya Jumatatu, alishangaa kwa nini kiongozi wa Azimio hawezi kushutumu maandamano kama hayo yanapogeuka kuwa ghasia.
  • Wahome ambaye anajiunga na orodha ya washirika wa Rais William Ruto ambao wametaka kukamatwa kwa kiongozi huyo wa upinzani ametaja vitendo vyake vya uhalifu.
WAZIRI ALICE WAHOME
Image: TWITTER

Waziri wa Maji na Usafi wa Mazingira Alice Wahome ametoa maoni yake kuhusu maandamano ya Azimio yanayoendelea akisema kiongozi wa Upinzani Raila Odinga anafanya mapinduzi na anafaa kukamatwa.

Wahome ambaye anajiunga na orodha ya washirika wa Rais William Ruto ambao wametaka kukamatwa kwa kiongozi huyo wa upinzani ametaja vitendo vyake vya uhalifu.

"Anafanya mapinduzi kwa serikali. Anafaa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka," Wahome alisema.

Katika ujumbe siku ya Jumatatu, alishangaa kwa nini kiongozi wa Azimio hawezi kushutumu maandamano kama hayo yanapogeuka kuwa ghasia.

"Haikubaliki kwa kiongozi kuitisha maandamano na inapotokea vurugu ambapo watu wanauawa na mali kuharibiwa, hana akili wala ulimi wa kulaani uharibifu," aliongeza.

Mpango wa kukusanya sahihi milioni 15 na Azimio ili kutengua utawala wa Ruto umewazonga viongozi wa Kenya Kwanza wanaodai Raila ana nia ya kusababisha machafuko.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei, Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala na Mbunge wa Kimilili Didmus Baraza ni miongoni mwa viongozi wengine ambao pia wameingia kwenye rekodi wakimshutumu Raila kwa kuzua fujo nchini.

"Kwa sisi tunaoamini katika utawala wa sheria, Raila na waandalizi lazima wakamatwe mara moja, kwa sababu anaendelea kuleta fujo, fujo na uharibifu wa mali," Cherargei alisema.

Malala alisema maandamano makubwa yamesababisha uhujumu uchumi.

Lakini, baadhi ya wabunge wa ODM wameonya serikali kumkamata Raila, wakisema kuwa jaribio lolote litayumbisha nchi.

"Nchi iko katika hatari ya kusambaratika iwapo lolote litatokea kwa Raila," Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alisema.

Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo kwa upande wake alionya kuwa serikali itawajibishwa iwapo lolote litatokea kwa Raila.

“Raila ni kitendawili katika nchi hii. Ikitokea lolote kwake achana na vitisho vya kumkamata, likitokea lolote kwake tutaiwajibisha serikali hii. Raila anafaa kuheshimiwa,” akasema.

 

 

 

 

 

View Comments