Baraza la kusimamia Vyombo vya Habari nchini (MCK) limewakosoa maafisa wa polisi kwa kujifanya wanahabari wakati wa maandamano yanayoendelea ya kupinga serikali.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano jioni, Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Owoyo alibainisha kuwa polisi wakijifanya wanahabari ili kuwakamata waandamanaji wakati wa maandamano yanayoongozwa na viongozi wa Azimio la Umoja ni tishio kwa kazi ya waandishi wa habari.
Hii ni baada ya afisa mmoja wa polisi aliyekuwa amevalia mavazi ya kawaida ambaye alijifanya kuwa mwanahabari ili kumlenga mwandamanaji katika eneo la Mathare, Nairobi mnamo Jumatano kunaswa na kamera.
"Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya limegundua kwa wasiwasi mkubwa visa vya maafisa wa usalama kujificha kama wanahabari wanaoripoti maandamano kwa nia ya kuwakamata waandamanaji," taarifa ya MCK ilisoma.
"Uigizaji wa waandishi wa habari na polisi ni utovu wa maadili ya kazi kwa upande wa polisi na unahatarisha maisha ya waandishi wa habari wakiwa kazini."
Chombo hicho cha habari kilibainisha kuwa wanahabari wote wanalindwa chini ya vifungu vya 33, 34 na 35 vya katiba na kuwataka polisi kuheshimu haki za wanahabari.
Kwa upande mwingine, Omwoyo hakukosa kuwathamini walinda sheria hao kwa kuwaachilia wanahabari kadhaa waliokuwa wametiwa mbaroni wakati wakiripoti maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi siku ya Jumatano.
"Wakati Baraza linashukuru kuachiliwa kwa waandishi wa habari ambao walikamatwa hapo awali wakati wakiripoti maandamano, kuwaweka kizuizini waandishi wa habari haukuwa wa lazima, wa kiholela na wa kejeli," ilisema taarifa hiyo.
Wakati wa maandamano ya Azimio siku ya Jumatano, afisa wa polisi bila sare alinaswa kwenye kamera akimvizia mwandamanaji na kisha kumkamata. Afisa huyo alikuwa amejifanya kurekodi matukio ya maandamano yaliyokuwa yakiendelea kwa kamera huku akimvizia mwanamume mmoja ambaye alikuwa akiwalalamikia polisi kwa madai ya kumrushia mtoto wake vitoa machozi.
Kufuatia tukio hilo, huduma ya polisi ilikosolewa sana na waandishi wa habari, wananchi na vyombo vingine.