In Summary
  • Hata hivyo, Kioni alidai, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakikodi majambazi kushambulia biashara za kibinafsi na kupora mali na kisha kulaumu Azimio.
Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee Jeremiah Kioni
Image: Jeremiah Kioni /TWITTER

Jeremiah Kioni amepuuzilia mbali madai kuwa waandamanaji wa Azimio wamekuwa wakiharibu mali wakati wa maandamano.

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa alisisitiza kuwa maandamano ya nchi nzima yamekuwa ya amani.

Hata hivyo, Kioni alidai, baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakikodi majambazi kushambulia biashara za kibinafsi na kupora mali na kisha kulaumu Azimio.

“Katiba inahakikisha haki ya kuandamana na badala ya waandamanaji kulindwa kutekeleza haki yao, wameuawa,” alidai Kioni.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Radio Jambo Jumanne asubuhi, Kioni alisisitiza kuwa Wakenya hawatatishika kufanya kile ambacho kimeainishwa na Katiba.

"Mauaji na uharibifu wa mali ambayo tumeshuhudia hayajafanywa na waandamanaji," Kioni alidai.

"Wakati wowote tumejitokeza kuandamana chini ya uongozi wa Raila, hakuna uharibifu wa mali umeshuhudiwa."

Hata hivyo, serikali imewashutumu wapinzani kwa kutumia wahuni kuharibu mali na pia kuhujumu uchumi wakati wa maandamano yao.

Serikali pia ilidai kuwa baadhi ya wanasiasa wa Azimio walikodi bunduki ambazo zilitumiwa kuwaua waandamanaji ili mauaji hayo yalaumiwe kwa serikali.

Upinzani ulifanya takriban mikutano 17 ya hadhara kote nchini kabla ya kuitisha maandamano ambayo yametikisa nchi hiyo katika muda wa miezi miwili iliyopita.

Jumatatu jioni, upinzani ulisitisha maandamano ya nchi nzima ambayo yalikuwa yamepangwa kufanyika Jumatano wiki hii.

Viongozi hao wa upinzani badala yake watawaongoza Wakenya katika msafara wa amani kuwasha mishumaa na kuweka maua katika maeneo maalumu kote nchini.

View Comments