In Summary

• Mwakilishi wa wazazi shuleni Elias Mberi alisema kuwa uamuzi huo ulifanywa katika mkutano wa wakuu wa shule hiyo, ili kupunguza utovu wa nidhamu kwa wanafunzi.

• Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Taita Taveta Khalif Hirey alikashifu uamuzi wa shule hiyo wa kuwataka wazazi kununua unga na mafuta ya kupikia.

Wanafunzi wakielekea katikati mwa jiji la Nairobi baada ya shule kufungwa.
Image: MAKTABA

Wanafunzi 10 wa shule ya sekondari ya Voi wametimuliwa shuleni kwa kula vipande vya ziada vya mkate wakati wa kula kiamsha kinywa.

Kulingana na ripoti ya Nation, wanafunzi hao ambao walitimuliwa shuleni humo siku ya Jumatatu walitakiwa kurejea shuleni wakiwa na unga wa ngano na lita 10 za mafuta ya kupikia kama adhabu.

Mwakilishi wa wazazi shuleni Elias Mberi aliambia Nation kuwa uamuzi huo ulifanywa katika mkutano wa wakuu wa shule hiyo, ili kupunguza utovu wa nidhamu kwa wanafunzi.

“Huo ndio utaratibu unaofanyika katika shule zote nchini, katika hali hii mzazi sasa atampa mtoto nidhamu, mtoto pia ataona mzazi amepitia wakati mgumu na hatarudia kosa hilo,” Mberi alisema.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Taita Taveta Khalif Hirey alikashifu uamuzi wa shule hiyo wa kuwataka wazazi kununua unga na mafuta ya kupikia.

Alisema musimamizi wa shule hiyo ilipaswa kutumia hatua mbadala za kinidhamu dhidi ya wanafunzi hao.

Hata hivyo, aliongeza kuwa ofisi yake haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa shule au wazazi.

Aidha aliwataka wazazi walioathirika kuripoti kisa hicho ofisini kwake na kuongeza kuwa tukio hilo litachunguzwa.

"Wazazi hawapaswi kukwepa kuja kwetu. Hatutawadhulumu kwa sababu wanatafuta haki. Hilo likitokea basi hatutaunga mkono vitendo vya aina hiyo vinavyofanywa na shule," alisema.

View Comments