In Summary

•Takriban watu 12 walipoteza maisha yao kufuatia ajali ya barabarani iliyofanyika Voi kwenye barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Mombasa.

• Wawili walipata majeraha makali ya kichwani huku mmoja akiwa na majeraha ya kifua.

Ajali ya barabarani Voi
Image: Hisani

 Watu 12 walipoteza maisha kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea Voi kwenye barabara kuu ya kutoka Nairobi kuelekea Mombasa siku ya alhamisi Septemba 7.

Ajali hiyo ilihusisha matatu yenye uwezo wa kubeba abiria 14, wakati ambapo ziligongana ana kwa ana na lori kupelekea vifo vya watu hao.

Akidhibitisha ajali hiyo, OCPD wa Voi Bwana Bernastain Shali, alisema kuwa, watu watatu akiwemo dereva wa lori hilo wamelazwa kwenye Hospitali ya rufaa ya kaunti ya Moi ambapo wanaendelea kupokea matibabu;

"Dereva wa lori na abiria wawili walipata majeraha mabaya na kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Moi,"

Akizungumza daktari Jeremia Shem ambaye anatoa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Moi, alisema wanafanya kila juhudi kushughulikia waiojeruhiwa.

Shem, alieleza kuwa, wawili walipata majeraha makali ya kichwani huku mmoja akiwa na majeraha ya kifua.

Mtu mmoja baadaye aliaga dunia akipokea matibabu na kufikisha idadi ya walioaga dunia kufikia 13.

Mtu mmoja aliyeponea kutokana na ajali hiyo ya mauti, alieleza jinsi alijinasua na kujaribu kumuokoa dereva;

"Chenye kilinisaidia, suruali yangu ilikua imeshikwa na mlango, baadaye nilipata fahamu nikajitoa hapa na kuamua kusaidia dereva juu alikua amelaliwa na kiti,"

Aidha Bwana Shari alieleza kuwa, matatu hiyo ilikuwa ikielekea Mombasa kutoka Nairobi huku lori likisafirisha mizigo kutoka Mombasa keulekea Juba, Sudan Kusini.

Mkuu huyo wa polisi vilevile amedhibitisha kuwa miili ya waathiriwa ilipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Moi.

Polisi wakishirikiana pamoja na shirika la NTSA wameahidi kufanya uchunguzi ili kubaini kiini cha ajali hiyo.

View Comments