In Summary

•Kenya Airways ilithibitisha katika taarifa yake ya Jumanne asubuhi kwamba tukio hilo lilitokea mwendo wa saa nane alasiri siku ya Jumatatu.

•Wahudumu wa ndege hiyo wakisaidiwa na madaktari wawili na muuguzi mmoja walitoa usaidizi wa kimatibabu kwa abiria huyo.

Image: HISANI// KENYA AIRWAYS

Ndege ya shirika la Kenya Airways iliyokuwa ikisafiri kutoka nchini humu kuelekea jiji la London, Uingereza siku ya  Jumatatu mchana ililazimika kutua kwa dharura baada ya mmoja wa abiria wake kuugua akiwa ndani ya ndege hiyo.

Shirika la Kenya Airways lilithibitisha katika taarifa yake ya Jumanne asubuhi kwamba tukio hilo lilitokea mwendo wa saa nane alasiri siku ya Jumatatu.

Kulingana na kampuni hiyo, wafanyakazi wa ndege hiyo wakisaidiwa na wahudumu watatu wa afya wakiokuwa kwenye ndege hiyo walitoa usaidizi wa kimatibabu kwa abiria huyo kabla ya ndege kutua kwa dharura kwa matibabu zaidi.

"Kenya Airways PLC (KQ) inathibitisha kwamba mnamo Jumatatu, tarehe 9 Oktoba 2023, mwendo wa saa 14:19 KQ100 iliyokuwa ikisafiri kutoka Nairobi hadi London Heathrow, ilitangaza dharura ya matibabu baada ya abiria kuugua," taarifa ya shirika la Kenya Airways ilisema.

Waliongeza, “Wahudumu waliokuwa ndani ya ndege hiyo wakisaidiwa na madaktari wawili na muuguzi mmoja walitoa usaidizi wa kimatibabu kwa abiria huyo huku nahodha akitangaza dharura ya kiafya kwa Kitengo cha Udhibiti wa Usafiri wa Anga (ATC) ili ndege hiyo iweze kutua kwa haraka kwa ajili ya abiria. kupata matibabu zaidi."

Kampuni hiyo ya ndege iliendelea kusema kuwa usalama wa abiria wao utaendelea kuwa kipaumbele chao daima.

View Comments