In Summary

•Watahiniwa, wazazi wao na walezi sasa wanaweza kupata matokeo kupitia tovuti ya KNEC, SMS ama katika afisi za elimu za kaunti na shule zao.

•Watahiniwa wanapaswa kutuma nambari yao ya usajili, zikifuatiwa na herufi kubwa KCPE (kwa herufi kubwa)  kwa 40054 ili kupata matokeo.

Waziri Ezekiel Machogu wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa KCPE 2023 katika jumba jipya la KNEC la Mitihani mnamo Novemba 23, 2023.
Image: DOUGLAS OKIDDY

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu ametangaza rasmi matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa KCPE 2023 ambayo yalikuwa yakisubiriwa kwa hamu.

Watahiniwa, wazazi wao na walezi sasa wanaweza kupata matokeo kupitia tovuti ya Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC), mfumo wa SMS ama katika afisi za elimu za kaunti na shule zao.

Kwa chaguo la SMS, watahiniwa wanapaswa kutuma nambari yao ya usajili (index number), ikifuatiwa na neno KCPE (katika herufi kubwa)  kwa 40054 ili kupata matokeo.

"Wazazi na watahiniwa wanaweza kupata matokeo yao ya KCPE kwa kutuma nambari zao za usajili kwa nambari 40054. SMS hiyo itatozwa Sh25," Waziri Machogu alisema.

Mfumo wa SMS unapatikana kwa huduma zote za simu na itatozwa Sh25 kila moja.

Mwaka huu, baraza lilisajili watahiniwa milioni 1.4 ikilinganishwa na watahiniwa milioni 1.2 mwaka 2022.

Huku akitangaza matokeo ya mwaka huu, waziri Machogu alisema mtahiniwa bora zaidi wa KCPE 2023 alipata alama 428 kati ya 500.

Machogu alitangaza kwamba ni watahiniwa 8,523 pekee waliopata zaidi ya alama 400.

“Idadi ya watahiniwa ambao walipata alama 400 hadi 500 ilikuwa 8,525 ambayo ni sawa na asilimia 0.60,” Waziri Machogu alisema.

Waliopata alama kati ya 300 hadi 399 walikuwa 352,782 ambayo ilikuwa 24.29%.

“Alama 200 hadi 299, watahiniwa waliokuwa katika kundi hilo walikuwa 658,278, ambayo ni asilimia 48.49,” alisema Machogu.

Waliopata kati ya alama 100 hadi 199 walikuwa 383,025, huku waliopata kati ya alama 0 hadi 99 walikuwa watahiniwa 2,060.

Huu ndio mwaka wa mwisho watahiniwa watafanya mitihani ya KCPE huku wizara ikijishughulisha na kumaliza mtaala wa 8-4-4.

View Comments