In Summary

• Nyoro alidai kuwa rais huyo wa zamani alikuwa na nia ya kupinga serikali ya Rais William Ruto kupitia maandamano.

Ndindi Nyoro.
Image: X

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ameanza mwaka 2024 kwa mwendelezo wa kile ambacho serikali ya Kenya Kwanza ilikuwa ikidai mwaka uliopita.

Mbunge huyo sasa amerejelea madai yake kwamba ana ufahamu fika kuwa rais mstaafu Uhuru Kenyatta ndoye yuko nyuma ya maandamano ya Azimio ambayo huenda yakafanyika tena mwaka huu ikiwa maneno ya Raila Odinga yatakuwa kweli.

Nyoro alidai kuwa rais huyo wa zamani alikuwa na nia ya kupinga serikali ya Rais William Ruto kupitia maandamano.

Mbunge huyo mtetezi mkali wa sera za Ruto alikuwa akiyasema haya huko Njabini kaunti ya Nyandarua wakati wa hafla ya kumzika babake seneta wa Nyahururu Methu John.

"Tunamtaka rais wa zamani, ambaye aliheshimiwa sana na Wakenya wakati wa uongozi wake, akome kutumia rasilimali zake kufadhili maandamano ya vijana na kesi mahakamani kupinga mradi wa ujenzi wa nyumba ambao hutoa ajira kwa vijana hawa," Nyoro alisisitiza.

Mbunge huyo alisema kuwa serikali haitaguswa na maandamano hayo yanayolenga kuwapendelea baadhi ya wanasiasa.

Akizungumza huko Kiharu, mbunge huyo alisema utawala wa Ruto hautatikiswa na vitisho vya Azimio kurejea mtaani.

Kenyatta awali alikanusha madai kwamba alikuwa akifadhili shughuli za Upinzani aliposhutumiwa mwaka jana kwa kufadhili maandamano ya mitaani dhidi ya serikali.

View Comments