logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Ichung’wah apendekeza nyadhifa za ugavana wa kaunti zitengewe wanawake pekee

Alimtaka Ruto kufanyia katiba marekebisho.

image
na Davis Ojiambo

Habari24 January 2024 - 06:32

Muhtasari


  • • Katika utafiti wa hivi majuzi zaidi, sehemu ya magavana wa kike iliorodheshwa miongoni mwa magavana kumi waliofanya vizuri zaidi nchini.
MP Kimani Ichung'wah

Mbunge wa Kikuyu ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung'wah amemtaka Rais William Ruto kufanya mabadiliko kwenye nafasi ya ugavana.

Akihutubia umati mnamo Jumanne, Januari 23, 2024, Ichung'wah alipendekeza kuwa wadhifa wa ugavana wa kaunti utengewe wanawake pekee.

Kulingana na Ichung'wah, pendekezo hilo likitekelezwa lingefaidi kaunti kwa sababu magavana wanawake wanafanya kazi vizuri zaidi kuliko wenzao wa kiume.

"Kama itafika siku uweze kubadilisha katiba, naona uibadilishe kiti cha ugavana kuwa cha hawa wamama kwa sababu wao ndio wanaelewa kazi hii ya ugavana," alisema.

Katika utafiti wa hivi majuzi zaidi, sehemu ya magavana wa kike iliorodheshwa miongoni mwa magavana kumi waliofanya vizuri zaidi nchini.

Kulingana na utafiti wa Infotrak mnamo Novemba mwaka jana, magavana wa kike kama vile gavana wa Homa Bay Gladys Wanga waliongoza orodha ya magavana 25 waliofanya vizuri zaidi kama gavana aliyefanya vyema zaidi nchini kwa asilimia 70.

Magavana wengine kama vile Kawira Mwangaza (Meru) walishika nafasi ya nane kwa 63%. Kinyume na hilo, Cecily Mbarire (Embu) aliorodheshwa wa 11 kwa asilimia 62, Wavinya Ndeti (Machakos) aliorodheshwa wa 13 kwa asilimia 61, huku gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru akiibuka wa 17 katika orodha hiyo kwa asilimia 59.

Utafiti huo ulifanyika kwa awamu mbili kati ya Julai na Septemba 2023.

Wakati wa utafiti wa kwanza, washiriki 36,200 walihusika ambapo uchunguzi wa pili ulihusisha washiriki 22,500.

"Utafiti wa pili uliohusisha washiriki 22,500 ulifanywa ili kuongeza ukubwa wa sampuli ili kila kaunti ndogo iwe na angalau wahojiwa 200," utafiti huo ulisema.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved