In Summary

• Aliagiza Wizara ya Utalii kuharakisha kuwalipa wadai 7,000 waliosalia waliothibitishwa na kulipwa Sh3 bilioni ndani ya siku 60 zijazo.

• Madai hayo ya fidia ni ya vifo, majeruhi, uharibifu wa mazao, uwindaji na uharibifu wa mali uliosababishwa na wanyama pori katika kata sita.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: KWA HISANI

Rais William Ruto ametangaza muda wa kufidiwa kwa familia za wananchi wanaouawa na wanyamapori haswa tembo kuwa ni miezi 6.

Akizungumza katika eneo la Rumuruti kaunti ya Laikipia Ijumaa wakati wa kuzindua mpango wa kufidia familia za watu waliouawa na tembo, Zaidi ya shilingi milioni 960, Ruto alisema kwamba kuanzia sasa kwenda mbele, mtu yeyote atakayeuawa na ndovu familia yake itafidiwa shilingi milioni 5 na serikali.

Rais alisema kulikuwa na takriban madai 17,000 ya fidia yaliyothibitishwa ya thamani ya Sh7 bilioni kwa kipindi cha 2014-2023 lakini serikali tangu wakati huo imelipa Sh4 bilioni kwa wanufaika wapatao 10,000.

Aliagiza Wizara ya Utalii kuharakisha kuwalipa wadai 7,000 waliosalia waliothibitishwa na kulipwa Sh3 bilioni ndani ya siku 60 zijazo.

Madai hayo ya fidia ni ya vifo, majeruhi, uharibifu wa mazao, uwindaji na uharibifu wa mali uliosababishwa na wanyama pori katika kata sita.

"Mwaka jana ilianzishwa katika Kaunti ya Taita Taveta, leo tumehamia Kaunti ya Laikipia na maagizo yangu ni kama ifuatavyo," alisema.

“Kufikia sasa tumefidia Sh4 bilioni kufikia mwisho wa fidia hii leo. Nyingine ambazo zinaendelea, karibu kesi 7,000 ambazo tayari zimethibitishwa, maagizo yangu ni kwamba tunapaswa kuwalipa fidia watu hao katika siku 60 zijazo.”

Rais alisema fidia ya haraka itajenga imani ya wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori na kuepusha uhasama kutoka kwa jamii wakati wowote wanyamapori wanapopotea katika makazi ya binadamu.

"Lazima tuwashirikishe wananchi katika uhifadhi kwa sababu wananchi kuwa katika msingi wa kila mpango kunahakikisha uendelevu. Pia tumefanya mabadiliko, hapo awali mtu akikatwakatwa na tembo hadi kufa, fidia ilikuwa Sh200,000. Sasa tumesema mwananchi akiuawa na tembo fidia ni Sh5 milioni,” Ruto aliongeza.

Alisema majeruhi kutokana na mashambulizi ya wanyamapori watalipwa kulingana na kiwango cha madhara ya wanyama hao hadi kufikia Sh4 milioni.

View Comments