In Summary

•Katika utabiri wa Jumapili, Met ilionya kuhusu mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo mengi ya nchi.

•Viwango vya mvua vinavyozidi milimita 30 vitakumba Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Nyanda za Juu Magharibi na Mashariki mwa Bonde la Ufa ikiwemo Nairobi.

Image: HISANI

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Kenya (Met) imetoa tahadhari kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa kuanzia Jumapili, Mei 19 Jumatano, Mei 22.

Katika utabiri wa Jumapili, Met ilionya kuhusu mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo mengi ya nchi.

Kufuatia hili, Wakenya wamehimizwa kuwa makini na kuangalia uwezekano wa mafuriko na kuongezeka kwa viwango vya maji katika vyanzo vya maji.

Viwango vya mvua vinavyozidi milimita 30 vitakumba Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Nyanda za Juu Magharibi na Mashariki mwa Bonde la Ufa ikiwemo Nairobi.

Kuanzia Jumatatu hadi Jumatano, viwango vya mvua katika maeneo yaliyo hapo juu vinaweza kuongezeka hadi 40 mm, Kenya Met ilionya. Kuanzia Jumatano kiwango cha mvua kinatarajiwa kupungua.

Hii itaambatana na upepo mkali mawimbi makubwa katika Bahari ya Hindi na upepo mkali katika ukanda wa mashariki.

Kaunti zinazoweza kushuhudia mvua kubwa ni pamoja na; Kisumu, Homabay, Siaya, Migori, Busia, Kisii, Nyamira, Nandi, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Narok, Baringo, Nakuru, Trans Nzoia, Uasin Gishu.

Nyinginezo ni; Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Turkana, Samburu, Nyandarua, Lakipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Nairobi, Machakos, Kajiado, Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale.

Madereva wa magari wamehimizwa kuepuka barabara ambazo maji yana viwango vikubwa ili kujiepusha na maafa.

“Watu katika maeneo yanayokabiliwa na maporomoko ya udongo hasa maeneo ya milimani wanapaswa kuwa waangalifu. Upepo mkali unaweza kuvuma paa, kung’oa miti na kusababisha uharibifu wa miundo,” mtaalam wa hali ya hewa aliongeza.

View Comments