In Summary

•Afisa wa polisi anayehusishwa na kituo cha polisi cha Kariobangi Kusini yupo hospitalini baada ya kujaribu kujiua kwa kunywa sumu.

•Afisa huyo alimwarifu mkewe,Jumapili 16,Juni 2024 kuwa alikuwa amepoteza bastola yake iliyokuwa na risasi 15.

Kitanzi
Image: HISANI

Afisa mkuu wa polisi anapigania maisha yake hospitalini baada ya kudaiwa kujaribu kujitoa uhai nyumbani kwake Ongata Rongai, kaunti ya Kajiado.

Inspekta wa polisi ambaye ni msimamizi wa kituo cha polisi katika eneo la Kariobangi  alikuwa amemwarifu mkewe Jumapili, Juni 16 asubuhi kwamba alikuwa amepoteza bastola yake rasmi aina ya Ceska iliyokuwa na risasi 15.

Mkewe aliambia polisi kuwa afisa huyo alionekana mwenye msongo wa mawazo alipofika nyumbani na kwamba hakukumbuka jinsi alivyopoteza silaha yake.

Afisa huyo aliripotiwa kujiachilia na kwenda katika eneo la kunawia mikono ,ambapo alimeza sumu. Familia ilimpata akihangaika baada ya kumeza sumu na kumkimbiza hospitalini.

Aidha,polisi wapo katika harakati za kutafuta silaha hiyo ila hawajafua dafu.Polisi walisema wanatembelea tena maeneo ambayo afisa huyo alitembelea saa zilizopita na kusababisha jaribio lake la kujiua.

"Hatua ifaayo imechukuliwa, na kikundi cha upekuzi kilitumwa kwa nyumba yake na maeneo ambayo alitembelea hapo awali," ripoti kutoka kwa polisi ilibaini.

Tukio hilo linaweza kuhusishwa na kiwewe, ambacho kinazidi kuongezeka miongoni mwa maafisa wengi wa polisi.Wengi wa maafisa wa polisi wamekufa kutokana na kujitoa uhai au kuua wengi katika hali inayohusishwa na msongo wa mawazo kazini.

Kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na hali hiyo, mamlaka za polisi zimezindua huduma za ushauri nasaha na tume ya kitaifa ya huduma ya polisi imeanzisha kitengo na kukipa wafanyikazi kushughulikia hali yao ngumu.

Kitengo cha ushauri nasaha, miongoni mwa mambo mengine, kitatathmini, kubuni na kuongoza programu ya kufikia watu ambayo husaidia kuzuia afya ya akili na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

View Comments