In Summary
  • Akizungumza na wanahabari nje ya Mahakama ya Milimani Jumanne, Kalonzo amewahakikishia Wakenya kwamba yeye, pamoja na viongozi wengine wa Azimio watahakikisha waliokamatwa wameachiliwa.
KALONZO MUSYOKA
Image: HISANI

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amelaani kukamatwa kwa watu kadhaa wanaoandamana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Akizungumza na wanahabari nje ya Mahakama ya Milimani Jumanne, Kalonzo amewahakikishia Wakenya kwamba yeye, pamoja na viongozi wengine wa Azimio watahakikisha waliokamatwa wameachiliwa.

Aliongeza kuwa wanaeleza haki zao na hawajaenda kinyume na katiba.

Aliongeza kuwa Mswada wa Fedha unawasilishwa wakati wa nyakati ngumu za kiuchumi kwa Wakenya.

"Wananchi wa Kenya wana haki ya kuandamana kwa mujibu wa katiba ya Kenya. Mswada wa Fedha umewasilishwa wakati ambapo Wakenya hawawezi hata kuweka chakula mezani na kwa hivyo, lazima wapiganie haki zao," Kalonzo alisema.

Kalonzo aliungana na mamia ya Wakenya kuomboleza kifo cha Hakimu Mkuu wa Makadara Monicah Kivuti ambaye alipigwa risasi na afisa wa polisi wakati wa kikao cha mahakama wiki jana.

Kikao hicho cha maombolezo kilifanyika nje ya mahakama za Milimani.

Katika hotuba yake, aliwataka majaji na mahakimu kufanyia kazi taarifa za kiintelijensia katika masuala wanayoyasimamia ili kuwawezesha kutoa haki wakiwa na uelewa wa kina nani wanamshughulikia mahakamani.

Wanachama kadhaa wa Idara ya Mahakama pia walituma risala zao za rambirambi kwa familia na marafiki wa Kivuti.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Igonga kupitia mwakilishi, Cynthia Nyamusi alisema Kivuti atakumbukwa kwa kujitolea kwake kutumikia watu kwa haki.

Aliahidi kufanya kazi kwa karibu na maafisa wengine wa mahakama ili kuhakikisha usalama wa watumishi wa mahakama na watumiaji wengine wa mahakama unaangaliwa na kufanyiwa kazi.

Chama cha Mahakimu na Majaji wa Kenya kilisema kuwa wamechoshwa na vitisho vinavyoelekezwa kwa maafisa wa mahakama na kwamba vyumba vya mahakama vinapaswa kuwa mahali salama kwao kutoa haki.

 

 

 

 

 

 

View Comments