In Summary

•Mwaliko kwa wanahabari kutoka kwa afisi ya DP, ambayo ilitajwa kuwa ya dharura, ilionyesha kuwa Gachagua atahutubia taifa kutoka kwa makazi ya Naibu Rais huko Kizingo, Mombasa.

NAIBU RAIS RIGATHI GACHAGUA
Image: DPCS

Naibu Rais Rigathi Gachagua leo saa kumi na mmoja unusu atahutubia taifa kutoka Mombasa.

Mwaliko kwa wanahabari kutoka kwa afisi ya DP, ambayo ilitajwa kuwa ya dharura, ilionyesha kuwa Gachagua atahutubia taifa kutoka kwa makazi ya Naibu Rais huko Kizingo, Mombasa.

Haya yanajiri huku Rais William Ruto akitarajiwa kuhutubia nchi kutoka Nairobi saa kumi jioni.

Hotuba za viongozi hao wawili zinajiri kufuatia wasiwasi mkubwa ulioibuliwa kuhusu msako mkali wa polisi dhidi ya kundi la vijana huko Githurai, Nairobi.

Mapema leo, Gachagua, wakati wa kongamano la wakuu wa shule, aliwaheshimu watu na polisi waliouawa katika maandamano.

Gachagua katika hotuba yake aliondoa siasa na Mswada tata wa Fedha wa 2024 ambao ulisababisha machafuko na vifo kote nchini.

Hata hivyo, aliwataka walimu wakuu wa shule za sekondari zaidi ya 8,000 wanaohudhuria kongamano la 47 la Wakuu wa Shule za Sekondari nchini Kenya (Kessha) katika ukumbi wa Sheikh Zayed, Mombasa, kusimama kwa dakika moja kuwaenzi waliofariki katika maandamano hayo.

"Kabla sijaongea, ninawaomba nyote muwe na utulivu kwa dakika moja kwa heshima ya watoto wetu na maafisa wa usalama, waliopoteza maisha katika maandamano ya jana na machafuko kote nchini," Gachagua aliwaambia wakuu wa Shule za upili.

Takriban watu 25 wameripotiwa kufariki kufuatia makabiliano kati ya polisi na waandamanaji katika miji yote mikuu ya Kenya.

Nairobi ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo ambapo takriban kesi 20 zimeripotiwa, baada ya wengi kuuawa kwa kupigwa risasi baada ya kuwazidi nguvu polisi na kuingia katika majengo ya Bunge.

Mjini Mombasa, watu watatu pia wameripotiwa kufariki.

Gachagua aliwasili Mombasa siku moja tu baada ya maandamano ya kupinga mswada wa fedha nchini kote.

View Comments