In Summary

•Nyamu alisema kuwa kukataa kwa Odhiambo kunazuia fursa ya kuwakilisha maslahi ya Wakenya katika ukaguzi wa deni.

•Jopo kazi hio ilipewa jukumu la kutathmini deni la taifa na kupendekeza masharti ya ulipaji

KAREN NYAMU
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu ameelezea kusikitishwa kwake na rais wa Chama cha Wanasheria nchini (LSK) Faith Odhiambo kwa kukataa uteuzi wa Rais William Ruto.

Rais Ruto alikuwa amemjumuisha Odhiambo katika jopokazi la kukagua deni la taifa.

LSK ilisema uteuzi huo kuwa kinyume na katiba.

Nyamu alisema kuwa kukataa kwa Odhiambo kunazuia fursa ya kuwakilisha maslahi ya Wakenya katika ukaguzi wa deni.

Katika mitandao ya kijamii, Nyamu alielezea mkanganyiko kuhusu uamuzi wa rais wa LSK kukataa uteuzi huo.

“Sina hakika ni kwa nini rais wa LSK Faith Odhiambo alikataa uteuzi wa Rais kwenye jopo kazi la ukaguzi wa kimahakama wa deni la umma. Alikosa nafasi ya kuhakikisha maslahi ya Wakenya yanawakilishwa na chama kikuu cha wanasheria.Ambao lengo lake ni kulinda na kusaidia umma katika masuala ya kisheria,”alisema.

"Deni la umma ni changamoto kubwa kwa nchi yetu, na nimesikitishwa kuwa hakutaka kuwa sehemu ya suluhisho." Aliongezea.

Rais Ruto alitangaza jopo kazi hilo mnamo Ijumaa, Julai 5.

Jopo kazi hio ilipewa jukumu la kutathmini deni la taifa na kupendekeza masharti ya ulipaji na mikakati ya mazungumzo, na kubainisha thamani ya miradi inayofadhiliwa na deni na mapato ya uwekezaji.

View Comments