In Summary

• Musyoka aliweka wazi kwamba yeye ameapa kusalia katika mrengo wa upinzani kuipinga serikali hadi pale udikteta utakapozikwa na demokrasia kunawiri.

KALONZO MUSYOKA

Kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ameweka wazi msimamo wake kwamba hatokubali kuketi kwenye mazungumzo ya kuunganisha taifa na serikali.

Akizungumza kwenye kongamano la vijana la Pan African kwenye shule ya sheria ya Kenya, kinara mwenza wa Azimio alisema kwamba kabla ya serikali kuanza kuzungumza kuhusu kuunganisha taifa kupitia mazungumzo, mwanzo wafanye haki kwa walioathirika katika maandamano.

Musyoka aliweka wazi kwamba yeye ameapa kusalia katika mrengo wa upinzani kuipinga serikali hadi pale udikteta utakapozikwa na demokrasia kunawiri.

“Kuhusu wazo la umoja wa kitaifa, suala ambalo rais Ramaphosa amesemma, nafikiri ndio njia ya kufuata, lakini sio hapa Kenya, samahani kwa kusema, sio sasa hivi. Tunaweza kuanza kufikiria kuhusu serikali ya umoja wa kitaifa kwenda mbele, pindi tu baada ya uchaguzi. Lakini sio kusubiri kwa miaka 2, watu wamekufa halafu unakuja kusema serikali ya umoja wa kitaifa? Sidhani ni wazo sahihi,” Musyoka alisema.

“Kwa hiyo kwa upande wangu, nimeweka wazi kwamba ninataka kuwa upinzani hadi pale tutakapoondoa udikteta katika taifa la Kenya.” Aliongeza.

Jumatano, Musyoka na chama chake cha Wiper walijitenga na wito wa kinara wa muungano wa Azimio Raila Odinga kutaka watu kuweka kando tofauti zao ili kuungana na serikali ya rais Ruto kuleta umoja na Amani.

Hii ni baada ya machafuko ya wiki mbili nchini baada ya vijana wa Gen Z kuandamana na kukabiliwa na polisi kaitka maeneo mbali mbali nchini.

Hata hivyo, rais Ruto aliwataka vijana kuacha maandamano ili kulipa suala la mazungumzo nafasi, jambo ambalo vijana wamepinga wakisema kabla ya mazungumzo, familia za waliokufa na wengine kutekwa nyara mwanzo zipate haki.

View Comments