MOSES KURIA
Image: HISANI

Aliyekuwa waziri wa utumishi wa umma, utendakazi, Moses Kuria ameanza kujuta kwa kile alisema ni kuwadharau vijana wa Gen Z ambao maandamano yao yalimpelekea kupoteza kazi kama waziri wiki jana.

Akizungumza na runinga ya Citizen, Kuria alisema kwamba alikuwa anawapuuza vijana wa Gen Z katika mtandao wa X lakini mwisho wa siku shinikizo zao zilimpelekea rais kulivunja baraza lake la mawaziri.

Kuria anasema kwamba katika maisha yake ya baadae kama atapata nafasi Mungu kumuuliza angependa kuwa nini, basi bila kusita atachagua kuwa Gen Z.

“Nimekuwa nikiwaita kizazi cha Uber na vidole vya samaki, wamenithibitishia kuwa sikuwa sahihi. Sasa wale watu nilikuwa naitwa kizazi cha uber na vidole vya samaki wamenionyesha kwamba wanaweza kuwa injini ya maana ya kulipeleka taifa mbele na kulirudisha kwenye njia salama. Kusema ukweli kama Mungu angeniambia nifunge macho yangu na nifanye ombi moja, ningeomba kuwa Gen Z,” Kuria alisema.

Moses Kuria alisema kwamba anaunga mkono mia kwa mia hatua ya rais kulivunja baraza la mawaziri, akisema kwamba kulikuwa na nyufa nyingi ambazo zilikuwa hata zinafanya kuwa vigumu kwa mikutano ya baraza la mawaziri kufanyika.

“Ni kweli tulikuwa na matatizo, hata kwa kufanya mikutano ya baraza la mawaziri ilikuwa ni shida, na ningependa kumpa rais nafasi ya kuunda upya  baraza lake la mawaziri, na kwa wenzangu, ningesema kwamba hatufai hata kusoneneka kwa lolote. Nafikiri nilimhurumia sana rais, na alikuwa ni lazima afanye chenye kilistahili kufanyika. Kama ni mimi kuachia nafasi yenye nilikuwa nashikilia ili tuwe na taifa, basi na iwe hivyo,” alisema.

Kuria pia alizungumzia suala la kukejeliwa mitandaoni baada ya baraza la mawaziri kuvunjwa na rais mnamo Julai 11.

“Naona watu wanani’enjoy eti ooh wewe ulifutwa, na hata hao wanajua, mimi ningependa kujizungumzia na kuzungumzia wengine, mimi sina majuto hata kidogo. Mimi huwezi nikuta kwenye kona eti ninalia kwa kupoteza kazi, hapana, mimi ni mtu wa kimataifa,” alisema.

View Comments