Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti ameitaka serikali kuipa kipaumbele vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia (GBV) kufuatia tukio la Kware.
Akitumia akaunti yake rasmi ya X Jumapili, Julai 14, 2024, Wavinya alisema kuwa serikali ya kitaifa inafaa kuimarisha ulinzi wa wanawake na mtoto wa kike ili kuzuia mauaji ya wanawake.
"Pia naiomba Serikali kuongeza ulinzi wa wanawake na mtoto wa kike na hasa kuweka kipaumbele katika mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia," alisema.
Akilaani mauaji ya kutatanisha ya wanawake, Wavinya alisema ni bahati mbaya kwamba miili ya wanawake iliyokatwakatwa vibaya iligunduliwa ikiwa imetupwa Kware Kaunti ya Nairobi.
Aidha Wavinya Ndeti ametaka uchunguzi ufanyike haraka na kukamatwa kwa wahusika.
“Ninalaani mauaji ya kutatanisha ya wanawake ambao miili yao imegunduliwa Kware, Kaunti ya Nairobi."
"Kama kiongozi mwanamke na mama, naomba uchunguzi ufanyike haraka kuhusu suala hilo na polisi wahakikishe wahusika watasakwa na kufikishwa mahakamani,” alisema.
"Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia zote zilizoathiriwa na tukio hilo la kusikitisha na ninatumai kwamba haki itatolewa hivi karibuni."
Mke wa Rais Rachel Ruto Jumamosi alivunja kimya kuhusu miili iliyogunduliwa katika mtaa wa Mukuru Kwa Njenga, Nairobi.
Rachel Ruto katika taarifa yake alisema kuwa kupatikana kwa miili ya wanawake wengi ilikuwa ya kutatanisha na kuhuzunisha.
Alitoa taarifa hiyo muda mfupi baada ya ripoti kuwa jumla ya miili iliyopatikana katika eneo la machimbo iliongezeka hadi 14 kufikia Jumamosi jioni.
“Kila mmoja wa wanawake hawa alikuwa mtoto wa mtu, dada au rafiki yake na hakuna mtu anayepaswa kufanyiwa ukatili huo. Unyanyasaji dhidi ya wanawake lazima ukomeshwe katika nchi yetu,” alisikitikia.
Mke wa rais alituma ujumbe wake wa rambirambi na maombi kwa familia za wahasiriwa huku uchunguzi ukiendelea kubaini wahusika wa uhalifu huo.
"Hakuna mzazi anayepaswa kumzika mtoto wao, haswa chini ya hali kama hii," ujumbe wake wa rambirambi ulisomeka kwa sehemu.