In Summary

•Uchunguzi unaendelea kuhusu jaribio la mauaji dhidi ya Trump, ambaye alionekana kwenye Kongamano la Kitaifa la Republican mjini Milwaukee siku ya Jumatatu.

•Ruto alimtakia Trump afueni ya haraka pamoja na familia za wahasiriwa wa shambulio hilo.

Rais William Ruto
Image: MAKTABA

Rais William Ruto amekashifu jaribio la mauaji kwa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump.

Akitumia mitandao ya kijamii, Ruto alitaja tukio hilo kuwa sio la kushtua tu bali pia la kuchukiza.

"Kwa niaba ya watu na serikali ya Jamhuri ya Kenya, ningependa kuongeza sauti yangu kwa wale wanaolaani jaribio la hivi karibuni la mauaji ya Rais wa zamani wa Marekani Donald J. Trump," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Ruto alimtakia Trump afueni ya haraka pamoja na familia za wahasiriwa wa shambulio hilo.

"Katika nyakati hizi za taabu, nachukua fursa hii kujitolea tena kwa maadili ya kidemokrasia tunayoshiriki na watu wa Marekani. Namtakia Trump afueni ya haraka na kamili," aliongeza.

Uchunguzi unaendelea kuhusu jaribio la mauaji dhidi ya Trump, ambaye alionekana kwenye Kongamano la Kitaifa la Republican mjini Milwaukee siku ya Jumatatu.

Trump alipigwa risasi sikioni wakati wa mkutano wa kampeni siku ya Jumamosi, katika shambulio lililoacha uso wa mgombea urais wa chama cha Republican ikiwa na damu.

Mpiga risasi alikufa, mhudhuriaji mmoja aliuawa, na watazamaji wengine wawili walijeruhiwa.

Baada ya tukio hilo,Katika chapisho kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump alisema risasi ilipenya "sehemu ya juu" ya sikio lake la kulia. Hapo awali, msemaji wake alisema "anaendelea vizuri" na anapokea matibabu katika kituo cha matibabu cha eneo hilo.

"Nilijua mara moja kuwa kuna kitu kibaya kwa kuwa nilisikia sauti ya mlio, milio ya risasi, na mara moja nikahisi risasi ikipasua kwenye ngozi," Trump aliandika. "Nilivuja damu nyingi, kwa hivyo niligundua kile kinachotokea."

View Comments