In Summary

• KWS ilitoa wito kwa umma kutipoti kisa chochote cha fisi wanaorandaranda mitaani kabla hawajazua maafa

SIKU YA FISI DUNIANI
Image: X//KWS

Siku moja baada ya taarifa za kuhuzunisha kuhusu mwanamke mchuuzi kushambuliwa na kuuawa na fisi eneo la Juja kaunti ya Kiambu, Shirika la wanyamapori limejibu.

Kupitia ukurasa wa X, KWS wametoa taarifa ya kuanzishwa msako mkali dhidi ya fisi huyo muuaji katika walikitaja kama oparesheni ya pili ya "ondoa fisi Juja".

"Katika kisa cha kusikitisha asubuhi ya leo, mwanamke mmoja alipoteza maisha yake kwa kushambuliwa na fisi katika eneo la Juja South Estate alipokuwa akitoka kufungua kioski chake cha chakula."

"Wakijibu haraka, Huduma ya Wanyamapori ya Kenya ilimtuma Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mahusiano ya Jamii na Ufikiaji, Bw. Abdi Doti, akiandamana na Afisa Mkuu Mwandamizi wa Mifugo Dkt. Bernard Rono na timu ya Hifadhi ya Kitaifa ya Oldonyo Sabuk kuhudhuria kesi hiyo na kutoa msaada," walisema.

Pia, Shirika hilo la wanyamapori humu nchini lilitoa rambirambi zake kwa marehemu ambaye alishambuliwa ba fisi akiwa njiani kwenda kuchuuza chakula.

"KWS inatuma rambirambi za moyo kwa familia iliyofiwa na kuahidi kuharakisha mchakato wa kufidia na kuahidi operesheni ya pili ya Ondoa fisi Juja inayoanza leo usiku. Wakaazi wa Juja South Estate wamehimizwa kuwa watulivu huku msako wa kina wa fisi hao wenye matatizo ukifanywa."

Itakumbukwa,  miezi michache iliyopita, KWS iliendesha oparesheni ya kwanza ya "ondoa fisi Juja" na shambulio hili ambalo limegharimu maisha ya mwanadamu linakuja kwa mshangao kwa wakaazi wa eneo hilo.

KWS ilitoa wito kwa umma kutipoti kisa chochote cha fisi wanaorandaranda mitaani kabla hawajazua maafa.

"Hivi majuzi KWS iliendesha Operesheni ya "Ondoa Fisi" huko Juja, pamoja na kampeni kali ya chanjo ya kichaa cha mbwa na ushirikishwaji wa jamii unaolenga kuzuia mzozo kati ya binadamu na fisi."

"Tunasalia imara katika kuhakikisha usalama na ustawi wa watu wa Juja kwa kufanya kazi na mashirika mengine yanayohusiana."

"Tunawaomba wananchi kuripoti matukio yoyote ya kunukuliwa kwa fisi," waliomba.

View Comments