Aliyekuwa gavana wa Kitui, Charity Ngilu amemtaka gavana wa sasa wa Kirinyaga Anne Waiguru kutolaza damu kisiasa na badala yake kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao, 2027.
Akizungumza katika kaunti ya Machakos wakati wa kongamano la viongozi wanawake kote nchini lililoandaliwa na mwenzao, Wavinya Ndeti, Ngilu alisema kuwa Waiguru ana tajriba ya kutosha kuongoza taifa.
Kauli ya Ngilu iliungwa mkono na gavana wa Kwale, Fatma Achani ambaye alisema ni wakati wanawake wa taifa hili kusimama na kuonyesha taifa uwezo wao katika uongozi wa juu zaidi kikatiba.
“Tunataka kuona mwanamke mmoja wa hapa Kenya akiwa rais wa Kenya. Amerika sasa inaenda kuwa na mwanamke [Kamala Harris] na wanawake wa Kenya wanaweza. Kwa hivyo, wewe Waiguru sasa unaelekea kutoka kwenye uongozi kwa sababu unamaliza miaka yako 10, angalia ni kiti kikubwa kipi utaingia. Na usiwe unaulizwa ni kipi, mbona si cha urais? Kwani kuna mtu mwingine anajua kushinda wewe? Umekuwa gavana, umekuwa waziri hivyo usitishwe, nenda mbele kwa sababu unaweza,” Ngilu alisema.
Itakumbukwa Ngilu aliweka historia nchini Kenya katika uchaguzi wa mwaka 1997 kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwania urais.
Katika uchaguzi huo hata hivyo, Ngilu hakufaulu kuingia katika ikulu baada ya kumaliza wa nne na kura 488, 600 kwa chama chake cha Social Democratic Part, SDP.
Uchaguzi huo ulishindwa na Hayati Moi wa chama cha KANU akifuatwa na Kibaki wa DP na nafasi ya tatu ikachukuliwa na Raila Odinga wa NDP.