In Summary

•Mwaura alithibitisha kupatikana kwa mili 19 ndani ya bweni lililoteketea huku watoto wawili wakifariki hospitalini.

•Kisa hicho kiliwaacha Wakenya wengi katika hali ya huzuni huku wakizifariji familia za waathiriwa wa mkasa huo wa moto.

Hillside Endarasha Academy ambapo wanafunzi 17 walifariki katika kisa cha moto mnamo Septemba 17, 2024.
Image: Wangare Mwangi// KNA

Idadi ya wanafunzi waliofariki kwenye mkasa wa moto uliotokea katika shule ya msingi ya bweni ya Hill Side Endarasha imefikia watoto 21 .

Siku ya Jumamosi, Serikali ya Kenya kupitia msemaji wake Isaac Mwaura ilisema watoto  wengine 17 hawajulikani waliko.

Mwaura alithibitisha kupatikana kwa mili 19 ndani ya bweni lililoteketea huku watoto wawili wakifariki hospitalini.

Siku ya Ijumaa asubuhi, Wakenya waliamkia habari za kusikitisha za mkasa wa moto ambao ulitangazwa kugharimu maisha ya takriban wanafunzi 17 katika shule ya msingi ya Hillside Endarasha Academy, katika Kaunti ya Nyeri.

Kisa hicho kiliwaacha Wakenya wengi katika hali ya huzuni huku wakizifariji familia za waathiriwa wa mkasa huo wa moto.

Wizara ya Elimu, katika taarifa yake Ijumaa asubuhi, ilithibitisha kuwa wanafunzi 17 walipoteza maisha huku wengine 14 wakiachwa na majeraha.

Hillside Endarasha Academy ni shule ya msingi ya wasichana kwa wavulana iliyoko Kieni Magharibi, katika Kaunti ya Nyeri.

Katika taarifa yake, wizara ya elimu ilibainisha kuwa shule hiyo ina wanafunzi 824, wavulana wakiwa 402 na wengine 422 wakiwa wasichana.

"Kati ya wanafunzi 824, wavulana 156 na wasichana 160 ni wa bweni, wakati wengine ni wasomi wa kutwa," PS wa Elimu ya Msingi, Belio Kipsang, alisema katika taarifa hiyo.

Kipsang alithibitisha kwamba wavulana wote 156 wa bweni walikuwa wakilala katika jumba ambalo liliteketea katika moto wa Alhamisi usiku.

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura alibainisha katika taarifa yake kuwa bweni hilo lilikuwa na wanafunzi wa darasa la 4–8.

Pia alithibitisha kuwa wanafunzi waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Mathari na Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyeri kupokea matibabu.

"Serikali imejitolea kikamilifu kusaidia waathiriwa, familia zao, na jamii pana ya shule katika wakati huu mgumu sana. Tunafanya kazi kwa karibu na mashirika yote husika, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Shirika la Msalaba Mwekundu, na washikadau wengine wakuu, ili kutoa usaidizi unaohitajika,” Mwaura alisema.

Pia alithibitisha kuwa misaada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vyakula vikavu, matandiko, vifaa vya tiba, vifaa vya huduma ya kwanza na huduma za ushauri nasaha vimepelekwa shuleni hapo.

View Comments