In Summary

• Genge la wezi wanaojifanya kuwa wahudumu wa matatu walikamatwa baada ya jaribio la kumpora abiria kutibuka.

• Mshukiwa mmoja mwanamke alifanikiwa kukwepa kutiwa mbaroni na maafisa wa DCI.

Pingu

Polisi kutoka kitengo maalum kwenye idara ya DCI imewakamata washukiwa 6 wanaoaminikia kuwahangaisha wasafiri wanaotumia usafiri wa umma katika jiji la Nairobi.

DCI imesema kuwa sita hao wamekuwa wakijifanya kuwa wahudumu wa matatu katika eneo la Parklands lakini nia yao imekuwa ya kuwaibia wasafiri , kuwateka nyara na baadaye kuwaachilia baada ya kutekeleza ujambazi.

Maafisa wa DCI kutoka kitengo maalum cha Operations Support Unit (OSU)  walifanikiwa kuwatia mbaroni washukiwa hao baada ya kuarifiwa na umma.

Inadaiwa kuwa genge hilo lilimbeba abiria mmoja katika eneo karibu na hoteli ya Villa Rosa Kempinski kabla ya kumwibia.

Wakati wa harakati ya kukamatwa kwa genge hilo, kutokana na wasiwasi ya kukamatwa na polisi, harakati hiyo ilisababisha ajali barabarani baada ya gari dogo kugonga mabango kando ya barabara.

Hata hivyo mwanamke mmoja anayedaiwa kuwa sehemu ya genge hilo alifanikiwa kutoroka  na wenzake ambao ni Boniface Wachiera Mwangi, Jackson Kimani Thuo, Dennis Omondi, George Vincent Otieno, Titus Mburu Njonjo  na John Waweru Njenga walikamatwa.

Aidha, maafisa hao wa OSU walifanikiwa kunasa simu tano na kipatakilishi kimoja kutoka na John Waweru. 

View Comments