In Summary

• Rais William Ruto ametembelea kikosi cha Kenya siku mia moja baada ya kikosi hicho kutumia nchini Haiti.

• Kenya inaongoza vikosi vingine vya polisi nchini Haiti katika mpango wa ujumbe wa msaada wa usalama  wa kimataifa maarufu kama MSS kurejesha utulivu nchini humo.

Rais William Ruto alipozuru kikosi cha Kenya nchini Haiti Septemba 21, 2024
Image: X//William Ruto

Rais Dkt. William Ruto Jumamosi alitembelea kikosi cha polisi wa Kenya waliotumwa nchini Haiti kuisaidia nchi hiyo kurejesha amani baada ya kushuhudiwa utovu wa usalama kutoka kwa magenge ya uhalifu wa ndani ya nchi hiyo.

Kenya ilituma jumla ya polisi elfu moja nchini Haiti katika mpango wa baraza la usalama la umoja wa mataifa UNSC kama sehemu ya ujumbe wa msaada wa usalama  wa kimataifa maarufu kama MSS kurejesha utulivu nchini humo.

Rais Dkt. Ruto alizuru nchi hiyo kutathmini maendeleo ya MSS, kutembelea na kupongeza kikosi cha Kenya kinachofanya kazi kwa ushirikiano na kikosi cha Haiti.

Alipotua nchini Haiti, Rais Ruto alipokelewa na baraza la rais la mpito likiongozwa na Edgard LeBlanc pamoja na baraza la mawaziri la Haiti.

Akihutubu katika ziara yake ya Haiti, Rais Ruto alisifia kikosi cha Kenya akiorodhesha mambo ambayo kikosi hicho kimefaulu katika taarifa aliyopewa na mamalaka ya nchini Haiti.

Dkt. Ruto alisema kuwa mamlaka ya Haiti ilimuarifu kuwa bandari kuu na uwanja mkuu wa ndege nchini Haiti umeanza  kufanya kazi na hivi karibuni uchumi wa nchi hiyo utaimarika.

Vile vile, Rais alisema kuwa shukle nchini Haiti zitafunguliwa kuanzia Oktoba Mosi ijapokuwa ufunguzi huo ulicheleweshwa. 

Kikosi cha Kenya kimeombwa kuzidi kushirikiana na kikosi cha Haiti kuhakikisha watoto wa Haiti wanapata fursa ya kupata elimu.

Baada ya ziara hiyo, Rais Ruto kupitia mtandao wake wa X alisema kuwa yuko tayari kufanya kikao na viongozi wengine wa dunia kujadili Haiti katika mkutano mkuu wa umoja wa mataifa utakaondaliwa baadsaye wiki hili.

Rais alikuwa ameandamana na mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi na balozi wa Kenya nchini Haiti Lemarron Kaanto.

 

 

View Comments