In Summary

• Wakati wa ziara yake, rais alikutana na maafisa hao zaidi ya 500 na kuanza mkutano wake nao kwa njia ya maombi.

• Kiongozi wa taifa alijitolea kuwapeleka mbele za Mungu ambapo aliombea usalama wao lakini pia akaliombea taifa la Haiti dhidi ya visa vya uchawi na kuabudu sanamu.

RAIS RUTO AKUTANA NA POLISI WA KENYA NCHINI HAITI.
Image: FACEBOOK//RUTO

Wikendi iliyopita, rais William Ruto alifanya ziara ya kushtukiza nchini Haiti kuwatembelea maafisa wa polisi wa Kenya ambao wamo nchini humo kwa oparesheni ya kurudisha Amani katika mitaa ya jiji kuu la Port-au-Prince.

Wakati wa ziara yake, rais alikutana na maafisa hao zaidi ya 500 na kuanza mkutano wake nao kwa njia ya maombi.

Kiongozi wa taifa alijitolea kuwapeleka mbele za Mungu ambapo aliombea usalama wao lakini pia akaliombea taifa la Haiti dhidi ya visa vya uchawi na kuabudu sanamu.

“Ninakuomba ewe Mungu wa mbinguni kwamba utawapa maafisa hawa ushindi ili waweze kurudisha Amani na kwa muda mfupi watarejea nyumbani baada ya kurejesha jukumu hilo kwa polisi wa Haiti. Baba tunataka kuomba dhidi ya uchawi na kuabudu sanamu na dhidi ya nguvu za gizani ambazo zimekalia taifa hili. Tunaomba kwamba utaikomboa Haiti kutoka mikononi mwa adui na kulifanya taifa hili kuwa la Amani,” Ruto alikariri maombi yake kwa sehemu.

Baada ya maombi, Ruto alijumuika na maafisa hao akiwafichulia kwamba alikuwa amewapelekea zawadi ya majani chai ya Kenya.

"Nimewaletea chai. Iko chai mingi hapa," alisikika akisema.

"Wapi Mutiso mtu wa logistics? iko chai nimeletea watu wako hapa. Watu wakunywe chai," aliongeza.

Majani ya chai yaliyopakiwa kwenye masanduku alikabidhiwa kwake na Monica Juma, Mshauri wa Usalama wa Taifa anayeambatana naye.

Ruto yuko Marekani kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa (UNGA) na alikuwa akizuru nchini kutathmini maendeleo siku 100 tangu kutumwa kwake.

 

View Comments