Chuo kikuu cha Moi chakabiliwa na uhaba wa kondomu
Afisa wa afya ya umma ametahadharisha wanafunzi dhidi ya kufanya mapenzi kiholela
• Wanafunzi wameshauriwa kuwa waaminifu katika mahusiano yao au kununua bidhaa hiyo muhimu madukani.
Chuo kikuu cha Moi jijini Eldoret kimewaonya wanafunzi wake kuwa kuna uhaba wa mipira ya kondomu katika chuo hicho.
Kupitia taarifa kwa wanafunzi kutoka kwa idara ya chuo cha sayansi ya afya chuo hicho kimeelezea kuwa kinakumbwa na uhaba mkubwa wa kondomu.
Taarifa hiyo ilitiwa sahihi na afisa wa afya ya umma P.I Sekenkei mnamo tarehe 19, Septemba iliwaonya wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho.
Onyo hilo linajiri siku chache baada ya kusajili wanafunzi wapya ambao wamejiunga na chuo hicho.
"Tunawajulisha kuwa kwa sasa hakuna mipira ya kondomu katika vituo vya afya ndani ya shule yetu." Chuo hicho kiliandika katika memo kwa wanafunzi.
Chuo hicho kimetaadharisha wanafunzi kujizuia wakiwa na uwezo, kuwa waaminifu kwa wapenzi wao na kujishughulisha katika mambo mengine wakati huu kunashuhudiwa uhaba wa kondomu.
Vile vile, wanafunzi wameshauriwa kununua bidhaa hizo madukani ikiwa watashindwa kujizuia ama watashindwa kuwa waaminifu katika mahusiano yao.