In Summary

•Familia ya Kapombe ilisema kuwa marehemu atazikwa nyumbani kwake katika eneo la Kikambala, kaunti ya Kilifi.

•Watu ambao wangependa kusaidia familia pia wametakiwa kutoa michango yao kupitia namba 4225832 (Patrick Kenga Kapombe).

Mashirima Kapmbe na marehemu mamake
Image: Instagram

Bi Angela Wanjala Kapombe, marehemu mama ya mwanahabari wa Citizen TV Mashirima Kapombe, atazikwa mnamo Oktoba 10, 2024, familia imetangaza.

Katika tangazo la mipango ya mazishi lililotolewa Ijumaa, familia ya Kapombe ilisema kuwa marehemu atazikwa nyumbani kwake katika eneo la Kikambala, kaunti ya Kilifi.

Mazishi ya Bi Angela Kapombe yatatanguliwa na hafla ya kuchangisha fedha na misa ya kutoa heshima za mwisho zitakazofanyika Septemba 27 na 28.

“Ni kwa huzuni kubwa tunatangaza kuondokewa na mpendwa wetu Angela Wanjala Kapombe. Familia na marafiki wanakutana kila siku nyumbani kwake Nyeri na Kikambala,” familia ilitangaza katika taarifa.

“Kutakuwa na uchangishaji fedha katika Kanisa Kuu la Watakatifu Wote siku ya Ijumaa tarehe 27/09/2024 saa 5.30 jioni na Misa ya Shukrani itakuwa katika Kanisa Kuu la Mama yetu wa Consolata, Nyeri Jumamosi tarehe 28/09/2024 saa kumi jioni.

Mazishi yatafanyika Alhamisi tarehe 10 Oktoba nyumbani kwake Kikambala, Kaunti ya Kilifi," Taarifa hiyo ilisomeka zaidi

Watu ambao wangependa kusaidia familia pia wametakiwa kutoa michango yao kupitia namba 4225832 (Patrick Kenga Kapombe).”

Mashirima alitangaza habari za kusikitisha za kifo cha mama yake mnamo Septemba 25 na kusema kuwa alikuwa amevunwa moyo na tukio hilo.

“Nimevunjika. Raha ya milele umpe mama, ee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie. Apumzike kwa amani. Amina,” alitangaza.

Mamia ya wanamtandao wakiwemo mastaa wenzake walimiminika kwenye akaunti yake na jumbe za rambirambi na kumtakia nguvu anapoomboleza mama yake.

Jumamosi asubuhi, mwanahabari huyo maarufu alitoa taarifa nyingine akiwashukuru wale wote ambao wameendelea kusimama naye katika nyakati hizi ngumu.

“Asanteni sana kwa simu zenu zote, maombi na ujumbe wa rambirambi, Asanteni kwa wote mliofanikiwa kufika kwenye mikutano ya Watakatifu Wote. Sasa tunahamishia kituo cha Nyeri kwa siku chache kabla ya kuendelea hadi Kikambala kaunti ya Kilifi,” akasema.

Mama yake Mashirima Kapombe alifariki dunia Septemba 25, 2025 akiwa na umri wa miaka 56.

View Comments