In Summary

•Waithera amepuuzilia mbali madai kuwa alifurushwa na kudai kuwa Hussein alikuwa akimsaidia kuruka juu ya jiwe lililokuwa limeziba njia yao.

•Alibainisha kuwa hakuwa amejiandaa kuhudhuria mdhahalo huo na alialikwa  masaa machache tu kabla ya kuanza.

Bi Pauline Waithera
Image: SCREENGRAB// JEFF KURIA TV

Mnamo Julai 27, video ilimuonyesha Mkuu wa Mawasiliano katika Sekretarieti ya Kampeni ya Ruto, Hussein Mohamed kama kwamba akimsukuma mwanamke mkongwe ilienezwa kwenye mitandao ya kijamii.

Tukio hilo lililotokea katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki mnamo usiku wa mdahalo wa urais lilizua hisia mseto mitandaoni huku wanamitandao wakiibuka na uchunguzi tofauti kuhusiana nalo.

Bi Pauline Waithera almaarufu Wambugua ambaye ndiye mwanamke anayedaiwa kusukumwa na mtangazaji huyo wa zamani hata hivyo amejitokeza kufafanua kuhusu yaliyojiri.

Ajuza huyo mwenye umri wa miaka 70 amepuuzilia mbali madai kuwa alifurushwa kwenye mkutano na kudai kuwa Hussein alikuwa akimsaidia kuruka juu ya jiwe lililokuwa limeziba njia yao.

"Kulikuwa na jiwe la urefu wa takriban futi moja unusu. Ingebidi tuzunguke ili kumfikia Ruto. Hussein aliona tungepoteza muda ikiwa tungeamua kuzunguka. Alinishika mkono wangu wa kulia kisha akanishika upande wa nyuma ili kunivukisha juu ya jiwe hilo," Bi Waithera alisema katika mahojiano na Jeff Kuria.

Alibainisha kuwa hakuwa amejiandaa kuhudhuria mdhahalo huo na alialikwa  masaa machache tu kabla ya kuanza.

"Hussein alinivukisha mara moja na kunisimamisha karibu na naibu rais. Hapo ndio inasemekana nilifurushwa, lakini alikuwa ananivukisha juu ya jiwe. Alinisukuma haraka ili nisimame karibu na mkubwa akihojiwa," Alisema.

Waithera alisema baada ya mdahalo kukamilika alirudishwa nyumbani na dereva aliyekabidhiwa jukumu la kumsafirisha.

Ajuza huyo alitumia fursa hiyo kuwaomba Wakenya kusita kuzungumzia yaliyojiri  kuhusu yaliyojitokeza katika hafla hiyo kwa niaba yake.

View Comments