In Summary

•Bosi huyo wa COTU alidokeza kwamba aliwahi kupatwa na hisia kuwa mgombea huyo wa Kenya Kwanza angekuwa rais.

•Atwoli aliwahimiza Wakenya wote kumkubali Ruto kama rais wao na kuipatia serikali yake muda wa kuwatumikia.

Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli
Image: CHARLENE MALWA

Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyikazi  (COTU) Francis Atwoli amebadilisha kauli yake kuhusu azma ya William Ruto ya urais.

Akizungumza siku ya Jumatatu baada ya Mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wa Ruto, Atwoli alikanusha kuwahi kusema kwamba naibu rais huyo anayeondoka hatawahi kuiongoza nchi ya Kenya.

Bosi huyo wa COTU alidokeza kwamba aliwahi kupatwa na hisia kuwa mgombea huyo wa Kenya Kwanza angekuwa rais.

"Kama nilivyosema siku zote, William ni mwanasiasa mahiri. Ndivyo nilivyokuwa nikisema. Lakini kama nilivyofikiria kwamba anaweza kuwa rais watano wa Kenya, sikusema hawezi kuwa rais," alisema katika mahojiano na NTV.

Atwoli aliwahimiza Wakenya wote kumkubali Ruto kama rais wao na kuipatia serikali yake muda wa kuwatumikia.

"Yeye ni rais wetu. Nawaomba Wakenya wote wa nia njema kusimama naye na kumpatia nafasi moja ya kuunda serikali yake, wamuunge mkono. Acha tumpatie muda tuone kama anaweza kufufua uchumi," alisema.

Aliweka wazi kuwa wakati alipokuwa akimpigia debe mshindani wa Ruto, Raila Odinga alikuwa akitumia haki yake ya kidemokrasia.

Jumatatu alasiri baada ya mahakama ya upeo kuamua kwamba uchaguzi mkuu wa Agosti 9 ulikuwa halali na ulifuata sheria, Atwoli alizamia kwenye mitandao ya kijamii na kumpongeza kwa ushindi.

Katika taarifa yake, alisema hatua ya kumpongeza mshindi baada ya hukumu ya mahakama ni uamuzi ambao ulifanywa wakati wa mkutano mkuu wa COTU.

"Wakati wa kikao cha  Bodi ya Uongozi  (K) mnamo tarehe 17 Agosti, tuliazimia kwamba mara tu baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu, lazima tumshukuru na kumpongeza mshindi. Kwa hivyo, tunampongeza Rais William Ruto," Atwoli alisema kupitia Twitter.

Bosi huyo wa COTU pia alichukua fursa hiyo kuwaomba wafanyikazi na Wakenya wote kwa ujumla kudumisha amani.

Kwa muda mrefu Atwoli amekuwa mkosoaji mkubwa wa Ruto. Amemkashifu hadharani mara nyingi na kumpigia debe Raila.

View Comments