In Summary

• "Kuna kitu kikali ndani yangu. Kitu chenye nguvu sana ndani..” - Karua.

Martha Karua, KIongozi wa NARC aandika mistari ya wimbo wa kuhimiza
Image: Twitter

Wakenya wamegawanyika katika makundi tofauti kuzungumzia hatua ya aliyekuwa mgombea mwenza wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Martha Karua kuachia mistari ya wimbo wa kuhimiza.

Juamanne, Karua aliachia mistari ya wimbo huo kwenye Twitter, hii ikiwa ni siku moja tu baada ya jopo la majaji saba wa mahakama ya upeo kutupilia mbali ombi lao la kutaka kubatilishwa kwa ushindi wa Ruto.

Ikumbukwe baada ya uamuzi huo wa mahakama, Karua alielekea kwenye Twitter na kuachia ujumbe wa kukubali shingo upande huku akisema kwamba hakubaliani na jinsi jopo hilo liliafikia uamuzi huo.

“Mahakama imezungumza. Ninaheshimu lakini sikubaliani na matokeo,” Karua alisema.

Kutoka kwa mishororo ya wimbo huo aliouandika kwenye Twitter yake, Karua aliashiria kwamba kulikuweko na kitu chenye nguvu na msukumo ndani yake ila anajua atatoboa majaribu hayo yote mwisho wa siku.

“Kitu chenye nguvu sana ndani, Ninajua kuwa naweza kuifanya. Ingawa unanifanya vibaya sana. Ulidhani kwamba kiburi changu kimepita, oh Hapana. Kuna kitu kikali ndani yangu. Kitu chenye nguvu sana ndani..” Karua aliandika kwenye Twitter yake.

Baada ya kuachia himizo hili katika wimbo ulioonekana kama tenzi ya rohoni, Wakenya wengi walikuwa na maoni kinzani kuhusu kile ambacho anakipitia katika muda huu ambapo azma yake ya kuwa naibu rais wa Kenya imetokomea hewani.

“Utabaki kuwa na nguvu sana, katika kiwango chako mwenyewe. Kwa sababu daima umesimama juu ya kile kinachozunguka ndani na nje! Tunaweka matumaini hai,” alimtia moyo aliyekuwa mgombea urais kwa wakati mmoja, profesa Ole Kiyiapi.

Sawa... Usilie basi,” mwingine kwa jina Felix Maina alimtania.

“Kwa upande wetu Mama hatutakuacha hata kidogo, tunaapa kuunga mkono na kufuata maelekezo yako. Tuko katika msaada wako bila kutetereka. Kuna matumaini mama. Haijaisha kwako na Baba,” mwingine alimtia moyo pia.

View Comments