In Summary

• Baada ya kumaliza, wengi walimsifia kwa kuitahidi katika Kiswahili na kujibu vizuri.

Seneta maalum Karen Nyamu amewachekesha wengi mitandaoni baada ya kupakia klipu akihojiwa na mwanahabari katika lugha ya Kiswahili.

Nyamu alihojiwa na mwanahabari wa runinga ya K24 katika lugha ya Kiswahili wakati wa kongamano la Maseneta uliofanyika Naivasha kaunti ya Nakuru.

Katika kile kiliwachekesha wengi, Nyamu alianza kujitetea mapema kwamba hakujua mwanahabari huyo angetumia lugha ya Kiswahili katika kumhoji, akidokeza kwamba japo lugha hiyo imekumbatiwa na wengi, kwake bado ni vigumu kujieleza kwa ufasaha kwa kutumia Kiswahili.

“Sikatai uko kazini lakini mbona unaniburuza na Kiswahili, kwa nini?” Nyamu aliandika kwenye klipu hiyo.

Mwanahabari huyo alitaka Nyamu kumueleza fika ni kwa nini labda Maseneta walihisi kwa kutoambiwa sababu za jaji mkuu Martha Koome kutoweza kufika huko Naivasha.

“Kwanza kabisa wakati unaniambia unataka kunihoji sikujua ni Kiswahili,” Nyamu alianza kwa kujitetea kabla ya mwanahabari kumwambia ako huru kutumia hata Kiingereza bora mawasiliano yaeleweke.

Seneta huyo alijitahidi kwa udi na ambari kujieleza katika lugha zote mchanganyiko wa Kiswahili na Kiingereza na hilo limewachekesha wengi mitandaoni.

“Kiswahili sio mdomo chetu.... Chapa mix,” Aphi Ashley aliandika.

Wengine walimpongeza kwa kuwa mkweli na kusema Kiswahili kwake ni vigumu kujieleza na kusema hata hivyo alijitahidi sana na kuzungumza vizuri katika lugha hiyo ya Afrika Mashariki.

Nyamu ni seneta maalum kutoka chama  tawala cha UDA.

View Comments