In Summary

• Mwili huo uliwasili katika uwanja wa ndege wa JKIA asubuhi ya Jumamosi na kupokelewa na watu wa karibu akiwemo babake.

Familia ya mwanamke aliyefariki katika hali isiyoeleweka mnamo Machi mwaka huu alipokuwa akifanya kazi nchini Saudi Arabia hatimaye imepokea mwili wake.

Akiweka wazi taarifa hizi, aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ambaye pamoja na timu yake ya Sonko Rescue walisimamia mchakato huo wa kusafirisha mwili wake kuja nchini baada ya kukwama kwa zaidi ya miezi saba alisema hatimaye dada huyo kwa jina Margret Ruguru Waweru atapumzishwa.

“Hatimaye tumefanikiwa kuleta mabaki ya Mkenya mwenye umri wa miaka 29 marehemu Margaret Ruguru Waweru. Margaret aliaga dunia mwezi Machi mwaka huu na mwili wake ulikuwa umelazwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Shimesi iliyoko Saudia Arabia kwa muda wa miezi 7 iliyopita. Mwili huo ulitua JKIA saa kumi na mbili asubuhi,” Sonko aliandika kwenye video hiyo ambayo alikuwa anaipeperusha moja kwa moja kupitia Facebook yake.

Margaret ambaye anatokea kaunti ya Nakuru kifo chake kilipotangazwa mapema mwaka huu ilikuwa sehemu ya takwimu za Wakenya wanaopitia wakati mgumu mikononi mwa waajiri wao Waarabu.

Miongoni mwa wale waliowasili katika angatua ya JKIA kupokea mwili wake ni babake ambaye aliwahi nukuliwa akisema kwamba siku kadhaa kabla ya kupokea ripoti za kifo cha bintiye, alikuwa ametishiwa na Mwajiri wake kwa kupoteza rimoti ya runinga.

Wengi walimpongeza Sonko kwa kuzidi kutoa misaada ainati kwa watu wanaohitaji misaada ya aina hiyo na kumshukuru kwa kuingilia kati kutatua mzozo uliokuwa umefanya mwili wa mwanadada huyo kuzuiliwa Uarabuni.

 

View Comments