In Summary

• “Namsihi Mudavadi, kwa vile ana thamani ya KSh bilioni 4 na huyu ni kakake, amruhusu achangie KSh bilioni moja ili Waluke aondoke gerezani,” Wanjala alitoa ombi kwa Mudavadi.

Wanjala amtaka Mudavadi kumsaidia Waluke.
Image: Facebook, maktaba

Mbunge wa Budalangi, Raphael Wanjala aliyejizolea umaarufu kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9 kwa kauli yake ya ‘Ruto Tawe’ amemuomba mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi kuingilia kati kesi inayomkumba mbunge wa Sirisia John Waluke na kumlipia faini ya bilioni moja anayodaiwa na mahakama.

Waluke ambaye amekabiliwa na kesi ya wizi wa mamilioni ya pesa katika hifadhi ya nafaka ya kitaifa NCPB alihukumiwa miaka 67 jela au kutoa faini ya shilingi bilioni moja.

Mapema mwezi Oktoba, mahakama ya juu ilidumisha uamuzi wa mahakama ambao ulimpa Waluke kibano cha miaka 67 jela au kulipa faini ya bilioni moja katika kesi hiyo iliyomhusisha na kupotea kwa milioni 313 kutoka mkoba wa NCPB.

Ikumbukwe hivi majuzi wakati wa kuhakikiwa bungeni, Mudavadi aliweka wazi kwamba utajiri wake ni wa thamani ya bilioni 4 na sasa Wanjala anamuomba kama mmoja wa viongozi kutoka ukanda wa Magharibi mwa Kenya kutoa japo bilioni moja katika hizo 4 ili kumlipia Waluke faini anayodaiwa.

“Namsihi Mudavadi, kwa vile ana thamani ya KSh bilioni 4 na huyu ni kakake, amruhusu achangie KSh bilioni moja ili Waluke aondoke gerezani,” Wanjala alisema katika mahojiano na kituo cha runinga cha TV47.

Jaji Esther Maina alisema mashtaka dhidi ya Waluke na Grace Wakhungu mbele ya Hakimu Elizabeth Juma yalithibitishwa bila shaka yoyote na kutakiwa kuchagua moja kati ya kulipa faini hiyo au kuhudumia kifungo cha miaka 67 jela.

"Adhabu hazikuwa nyingi. Ziko ndani ya sheria. Hukumu na hukumu zimethibitishwa," hakimu alisema.

View Comments