In Summary

• Huo ni uamuzi wangu wa kibinafsi na mtu hawezi kunilazimisha kuamini vinginevyo - Karua.

Karua asisitiza msimamo wake kuwa Ruto hakushinda urais
Image: Screengrab//YouTube

Kinara wa chama cha NARC Martha Karua ambaye pia alikuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais kupitia tikiti ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya amesisitiza msimamo wake kuwa hawezi kumtambua William Ruto kama rais wa Kenya.

Katika moja ya mazungumzo ya kipekee na kituo kimoja cha redio humu nchini, Karua alisema kwamba katu hawezi kushrutishwa kumkubali Ruto kama rais wakati fikira zake zinamueleza kwamba rais hakushinda kwa njia halali.

Mtangazaji alimtuia swali la kutaka kujua ni kwa nini kwa mara kadhaa katika mahojiano hayo alikuwa anamtaja Ruto kama naibu rais mstaafu na wala si rais na ndipo alijibu kwamba hawezi kulazimishwa kubadili fikira na mawazo yake kuhusu kile anahisi kilitokea katika uchaguzi wa Agosti 9.

“Sheria inamtambua kama rais lakini mimi simtambui hivo. Bado mimi nashikilia msimamo wangu kwamba yeye ni rais kisheria lakini mimi sina haja ya kulimbikizia sifa wadhifa ule. Nilisema niliheshimu uamuzi wa mahakama lakini sikukubaliana nao hata kidogo. Bado nasimama hapa kusema kwamba matokeo ya urais yaliingiliwa,” Karua alisema.

Aidha kiongozi huyo wa muda mrefu anayejulikana kwa misimamo tisti alizidi kujitetea kwa kusema kwamba huo ndio uamuzi wake kibinafsi na  wala hapatatokea mtu kumbadili kifikira.

“Huo ni uamuzi wangu wa kibinafsi na mtu hawezi kunilazimisha kuamini vinginevyo. Nazungumzia kuhusu kuamini kwangu binafsi na kuamini kwangu hakuna uhusiano wowote na sheria bali kuna uhusiano na fikira zangu. Bado nitazidi kusema kwamba Ruto hakushinda urais, basi tu!” Karua alisisitiza.

Alidokeza kwamba mpango wake wa kuendelea kusukuma ili kupata ukweli na haki katika mahakama ya ukanda wa Afrika Mashariki bado utaendelea hata kama waliheshimu uamuzi wa mahakama kutupilia nje ombi lao lililolenga kubatilishwa kwa ushindi wa rais Ruto.

View Comments