In Summary

• Ni sharti tuweke pembeni kurushiana lawama ili kutoa huduma kwa watu wa Kenya kutoka wadhifa wowote tunaoshikilia - Mudavadi.

DP Gachagua na mkuu wa mawaziri Mudavadi
Image: Facebook

Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi amewaambia baadhi ya viongozi waliochaguliwa kuweka siasa za kulaumiana pembeni na badala yake kuwafanyia wananchi waliowachagua kazi.

Mudavadi ambaye alikuwa anazungumza katika kaunti ya Machakos ambako aliongoza shughuli ya kusambaza chakula cha msaada kwa wahanga wa ukame alionekana kumrushia dongo naibu rais Rigathi Gachagua ambaye kwa muda mrefu amekuwa akimnyooshea kidole cha lawama kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga.

Mudavadi alisema kuwa karata za kutupiana lawana kutoka pande moja au nyingine zitaisha hivi karibuni na huenda ziishe kama ambavyo wengi hawakuwa wanaamini wala kutarajia na hivyo kuwataka viongozi wenzake serikalini kuwajibika katika kufanya kazi kwa wananchi.

“Na mimi nataka nisisitize kwamba baada ya uchaguzi, shida ziko. Tuweke mambo ya uchaguzi nyuma kidogo kwa sababu hata tukiendelea na kurushiana lawama, hatutasaidia. Mamlaka yamepewa na wananchi kwa wale wako kwa nyadhifa mbali mbali. Kwa hiyo sasa ni sharti tuweke pembeni kurushiana lawama ili kutoa huduma kwa watu wa Kenya kutoka wadhifa wowote tunaoshikilia,” Mudavadi alisema.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa walihisi kwamba matamshi haya yalimlenga naibu rais Rigathi Gachagua ambaye wikendi iliyopita na hata katika hotuba zake za awali ameonekana kumlaumu Odinga kwa madhira yaliyotendwa na serikali iliyopita.

Gachagua amekuwa akimzima Odinga kwamba hafai kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza kwani mambo ambayo wanaendelea kuyanyoosha ni kutokana na makossa ambayo yalitendeka katika kipindi cha pili cha serikali ya Jubilee baada ya Handshake ambayo Kenya Kwanza wanahisi muingiliano wa Odinga serikalini ulivuruga mipango mingi ya maendeleo kwa wananchi.

View Comments