logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Najua GMO itafanya tupoteze kura kiasi, lakini tutaona ufalme wa Mungu - Moses Kuria

Waziri alisema Kenya itaendelea kuagiza chakula kutoka nje kwa miezi 6 ijayo.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri18 November 2022 - 12:50

Muhtasari


• Najua hili litawaudhi baadhi ya watu lakini tutafanya hivi kama serikali. Hata kama tutapoteza kura kiasi hapa na pale lakini tutaona ufalme wa mbinguni - Kuria.

Waziri wa biashara, viwanda na uwekezaji Moses Kuria kwa mara ya kwanza ametilia kwenye mizani suala la serikali ya Kenya kuruhusu vyakula vya GMO nchini.

Katika video moja ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Kuria alisikika akitoa sababu zilizoifanya serikali kuruhusu vyakula vya GMO kutumiwa nchini licha ya pingamizi na wasiwasi kuibuliwa kutoka baadhi ya makundi yakiongozwa na viongozi wa kidini wanaosema vyakula vya GMO vinaenda kinyume na kazi ya Mungu aliyeumba vyakula kihalisia.

Kuria alisema kwamab nchi hii itaendelea kuruhusu vyakula hivyo nchini kwani hukua kwa kasi na haraka mno na hiyo ndio njia pekee ya kulikabili janga la njaa ambalo limewaathiri mamilioni ya Wakenya.

Kulingana na waziri, vyakula vya GMO havitakuwa njia ya kuua watu kwani kuna mambo mengi yanayoweka Wakenya katika hatari ya kupoteza maisha ikiwemo njaa yenyewe kutokana na kiangazi.

“Tuna vitu vingi sana ambavyo vinaweza tuua katika nchi hii. Kuwa katika taifa la Kenya moja kwa moja wewe ni mtahiniwa wa kifo. Na kwa sababu kuna vitu vingi vinashindana kutuua, tuliona tujumuishe vyakula vya GMO katika kundi hilo kimakusudi,” Kuria alisema huku watu wakicheka.

Kando na hapo, waziri pia alisema Kenya haijafikia kiwango cha kujisimamia kwa chakula na ndio maana yeye kama waziri wa biashara na viwanda ataruhusu shehena ya vyakula kuendelea kuagizwa kutoka nje ya nchi bila tozo ili kukidhi mahitaji ya Wakenya wengi wanaoungulia njaa.

Alisema kwamba hatua hiyo huenda itawauma baadhi ya Wakenya wafanyibiashara lakini itabidi hata kama itaisababishia serikali ya Ruto kupoteza kura bora kesho waingie peponi.

“Mpaka pale tutakapopata hakikisho kuwa tuna mahindi ya kutosha humu nchini, kesho nitatia saini katika notisi ya gazeti la serikali kukubalia kuagizwa kwa shehena ya mahindi gunia milioni 10 bila tozo kwa miezi sita ijayo mpaka pale tutakapojitosheleza kwa chakula. Najua hili litawaudhi baadhi ya watu lakini tutafanya hivi kama serikali. Hata kama tutapoteza kura kiasi hapa na pale lakini tutaona ufalme wa mbinguni,” Kuria alisema kwa utani.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved