In Summary

• Alisema kuwa serikali kwa ushirikiano na makanisa mbalimbali, watahakikisha mtoto wa kiume naye anapewa fursa ya kufurahia maisha.

Mama Dorcas Gachagua
Image: Facebook

Mke wa naibu rais Mama Dorcas Gachagua kwa mara nyingine amesisitiza haja ya kuwasaidia na kuwakimu kimaisha na kielimu watoto wa kiume kama ambavyo wale wa kike wanavyoshughulikiwa.

Mama Dorcas alikuwa anazungumza na wanahabari baada ya kuongoza ibada katika Kanisa la New Life huko Nyeri. Alitangaza kuwa kanisa litashirikiana na serikali kuanzisha mpango wa kuwawezesha wavulana.

Mama Dorcas anataka makanisa kuwa kimbilio salama kwa wavulana ambao wameacha shule na kujihusisha na utumizi wa dawa za kulevya. Kulingana na taarifa katika jarida la Nation, mama Dorcas alisema kuwa wavulana kwa miaka mingi wamepuuzwa na jamii, hivyo basi haja ya serikali kupeleka madaktari wa magonjwa ya akili na wanasaikolojia kuwarekebisha makanisani.

"Kama kanisa, tunahisi ni wakati wa kufuatilia tena hatua zetu na kuelekeza hatima zao na kuzipanga ili wapate kusudi katika maisha yao. Kanisa na serikali itahakikisha kwamba wavulana wanaokabiliwa na uraibu wa dawa za kulevya wanarekebishwa. Kanisa litatoa vipindi vya lishe ya kiroho na ushauri,” mama Dorcas alisema.

Alisema kuwa serikali kwa ushirikiano na makanisa mbalimbali, watahakikisha mtoto wa kiume naye anapewa fursa ya kufurahia maisha sawa na firsa sawa za kielimu kama ambavyo yule wa kike anashughulikiwa.

Alisema serikali itaanzisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa njia ya simu (TVet) katika makanisa ya msingi ili kuwafikia watoto walio katika mazingira magumu zaidi.

“Kama mama, nahisi huu ni wakati mwafaka wa kuchukua hatua. Kila kanisa litapatikana kwa ajili yao na ninatetea haki za mtoto wa kiume katika ofisi ya Second Lady,” Nation walinmnukuu mama Dorcas.

Alisema mpango huo utaibua ajira zaidi kwa vijana na kukomesha visa vya itikadi kali. Alitoa changamoto kwa kanisa kuwa tayari kukumbatia mpango huo badala ya kuwaweka kando watoto ambao wamekuwa wakiteseka mitaani.

View Comments