In Summary

• Cherera anajiuzulu siku mbili tu baada ya kamishna Justus Nyang’aya pia kung’atuka.

• Seneta huyo ambaye ni mwandani wa rais Ruto alisema kujiuzulu kwake kumelemaza kabisa hatua ya kinara wa upinzani Raila Odinga kuandaa maandamano.

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei
Image: Facebook//Cherargei

Seneta wa kaunti ya Nandi Samson Cherargei ametoa maoni yake punde baada ya naibu mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, Juliana Cherera kutangaza kujiuzulu wadhifa wake.

Cherera anajiuzulu siku mbili tu baada ya kamishna Justus Nyang’aya pia kung’atuka huku kukiwa na shinikizo kali kwa makamishna wane waliojitenga na matokeo ya urais wa Agosti kuachia ngazi.

Tayari rais Ruto amewasimamisha makamishna hao kazi kufuatia ripoti iliyowasilishwa kwake na kamati ya uchunguzi dhidi ya vitendo vyao ya JLAC mwishoni mwa wiki jana.

Cherargei anasema kujiuzulu kwa Cherera kama naibu mwenyekiti ni hatua ambayo imekuja kuchelewa kwani ndio umauzi ambao alifaa kuuchukua kitambo kabla hata ya kubuniwa kwa tume ya JLAC kuchunguza vitendo vyao vya baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Seneta huyo ambaye ni mwandani wa rais Ruto alisema kujiuzulu kwake kumelemaza kabisa hatua ya kinara wa upinzani Raila Odinga kuandaa maandamano ya kuwatetea makamishna hao Jumatano wiki hii.

Cherargei anasema Odinga hafai kupewa ulinzi wakati wa mkutano wake wa Jumatano wiki hii katika uwanja wa Kamkunji kwani Wakenya wanahitaji kufanya kazi na wala si kupewa ulizni wakienda kuandamana kwa sababu ya makamishna wane tu – ambao tayari wawili wameng’atuka tayari.

“Kujiuzulu kwa makamishna wa IEBC naibu Cherera na Ngang’aya kumecheleweshwa kwa muda mrefu baada ya kuiweka nchi katika hali ya machafuko na kumeweka Maandamo ya Tinga kwenye utata, mkanganyiko na kusahaulika kisiasa. Serikali imnyime kibali cha polisi sababu wakenya wanahitaji kufanya kazi,” Cherargei alisema kwenye tweet yake.

Makamishna wa IEBC naibu mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi walijitenga na matokeo ya kura za urais kwa kumtuhumu mwenyekiti Wafula Chebukati kuwa alikuwa na njama fiche ambayo hawakuielewa.

Na huo ndio ulikuwa mwanzo wa masaibu yake haswa baada ya rais Ruto kutangazwa mshindi na kuidhinishwa na jopo la majaji saba wa mahakama ya upeo, wakiongozwa na jaji mkuu Martha Koome.

View Comments