In Summary

• Alisema kuwa watatu hao waliingilia majukumu ya maajenti katika kituo kikuu na hapo ndio kila kitu kilianguka.

Odinga akiwa na huzuni
Image: Maktaba

Aliyekuwa agenti mkuu wa kampeni za kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, wakili Saitabao Ole Kanchory kwa mara ya kwanza amezungumza kiini kilichosababisha Raila Odinga kupoteza kura za urais.

Akizungumza katika Makala ya kipekee ambayo yalipeperushwa usiku wa Jumatatu katika runinga ya NTV, Ole Kanchory alisema kuwa kuna baadhi ya watu ambao waliingilia majukumu ambayo hayakuwa yao na hivyo kulemaza kampeni hizo.

Wakili huyo ambaye alikuwa agenti mkuu wa kusimamia kuhesabiwa kwa kura za urais kwa faida ya Odinga aliwataja watu watatu ambao walichangia kwa kiasi kikubwa Raila Odinga kupoteza kura.

Alisema mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya kampeni za Odinga, msomi profesa Makau Mutua na aliyekuwa waziri wa ICT Joe Mucheru walikuwa visingiti vikubwa katika safari ya Odinga kuelekea ikulu.

“Tulienda vibaya wakati tuliondoa baadhi ya taratibu kwa sababu kamati ya kampeni ilikuwa inafaa kuendesha karibia kila kitu lakini wakati fulani kamati hiyo ilinyofolewa pole pole na baadhi ya watu ambao walikuwa na ajenda zao binafsi. Hatungepoteza kura hizi kama si kwa watu watatu – Junet Mohammed, Joe Mucheru na Makau Mutua,” Ole Kanchory alifunguka.

Aliendelea kusimulia majukumu yao ambayo waliyaasi na kuingilia yasiyowahusu, hatua ambayo ilimpotezea Odinga nafasi ya kuwa rais baada ya kufanya majaribio mara 4 awali na hiyo ilikuwa safari ya tano akijaribu kuwa rais.

“Junet Mohammed ni mwanaume mmoja ambaye alitaka kujua kila kitu, na alipuuzilia mbali kila kitu mtu yeyote alisema. Alihakikisha kuwa hakuna mtu ambaye angekaribia Odinga, hata kama ni yule wa kumsaidia. Mucheru hakuwa na jukumu lingine mbali na kudidimiza shughuli za maajenti. Alikuja ndani kuangusha shughuli ya ajenti wetu, na alifanikiwa katika hilo. Makau Mutua alipowekwa kuwa kiongozi wa senta yetu ya kuangalia kura, basi ndio kila kitu kilianguka,” Ole Kanchory alifunguka huku akisema kuwa mengi ameyazungumzia katika kitabu chake.

View Comments