In Summary

• Picha ya mtawa huyo ilisambaa wiki chache zilizopita ambapo watu walikuwa wanaigeuza kichekesho kuwa ni mjamzito.

• Kanisa katoliki lilisema mtawa huyo anaugua lakini waliokuwa wanacheka hawawezi elewa tatizo lake.

Archidiocèse de Yaoundé
Image: Facebook

Wiki chache zilizopita , picha ya mtawa wa kanisa katoliki ilisambazwa pakubwa mitandaoni watu wakisema kuwa alikuwa mjamzito.

Mtawa huyo aliyeonekana katika picha amesimama na watu wengine huku tumbo lake likiwa limejitokeza mbele, jambo lililoashiria kuwa kuwa mjamzito na kuanza kufanyia picha hiyo utani mitandaoni.

Utani wenyewe ulijiri kutokana na dhana kwamba watawa na mapadre wa kanisa katoliki hawafai kujihusisha na vitendo vyovyote vya kujamiiana kwani wanapoingia katika huduma hiyo wanakula kiapo cha imani kutoa miili yao kumtumikia Mungu na wala si kushiriki vitendo vya mapenzi.

Wiki moja mbele,ilibainika kuwa picha hiyo ni ya mtawa mmoja anayehudumu katika taifa la Cameroon.

Kanisa katoliki katika taifa hilo la Afrika ya Kati limejitokeza wazi na kuzungumzia picha hiyo huku wakiwahurumia waliokuwa wanasema mtawa huyo ni mjamzito.

Kulingana na taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa dayosisi ya jiji kuu la Yaounde, mtawa huyo si mjamzito kama ambavyo watu walikuwa wanasema bali anaugua hali iliyopelekea tumbo lake kufura. 

Kanisa hilo lilimtaka Mungu kuwasamehe wote waliosambaza jumbe za kumkejeli kuwa mtawa huyo ana mimba, kwani walitumia mitandao yao kupata umaarufu kwa kuchafua jina la Mtumishi wa Mungu.

“Upotovu unapovamia ulimwengu, hakuna nafasi iliyobaki kwa kejeli na usemi ulioambukizwa...Kwa sisi sote tunaoshtushwa na posti zisizo na staha kuhusu huyo dada, Mola atupe nguvu ya kusimama na kumponya dada huyo,” Dayosisi hiyo iliandika.

Wanamitandao walimhurumia mtawa huyo na kuponda wale wanaotumia picha yake kutaka umaarufu mitandaoni wakisema kuwa ni kioja kuona mtawa mjamzito.

“Kweli huyu ni mgonjwa lakini watu wanatafuta jumbe zenye utashi ili kuendelea kumkejeli. Wacha Mungu awahurumie na sote tuungane kumuombea mtawa huyu kupona,” Larentine Atangwa alisema.

“Afya njema kwako dada Mungu aliweke neno lako karibu na wanaochafua sura yako,” Emma Parfaite alisema.

 

View Comments